K. M a r k s , F . E n g e l s

 

MAELEZO YA CHAMA CHA KIKOMUNIST

 


Tarehe ya kuandika: Katika 1847, kwa Karl Marx na Friedrich Engels.
Tarehe ya kuchapishwa: Katika februari 1848.
Toleo hili: Marxists Internet Archive (marxists.org), februari 2013.
Chanzo cha Nakala: Karl Marks na Frederick Engels, Maelezo y Chama cha Kikomunist, Moscow, Idara ya Maendeleo (1965).


 

 

Ulaya imepanda pepo - pepo wa ukomunist. Madola yote ya Ulaya ya zamani yameingia katika muungano mtakatifu kumpunga pepo huyu: Askofu mkuu wa Rumi na mfalme wa Urusi, Metternich na Guizot,[1] wageuzaji mambo wa Kifaransa na maaskari kanzu wa Kijerumani.

Wapi ambako chama cha upinzani hakikupata kuitwa cha Kikomunist na chama chengine chenye serikali? Wapi ambako chama cha upinzani hakikuvitupia vyama vingine vilivyoendelea mbele zaidi na vile vile maadui zake wapingao maendeleo lawama za kubandikwa jina la ukomunist?

Mambo mawili yanatokana na ukweli huo.

Ukomunist umeshaanza kukubaliwa na mamlaka zote za Ulaya kuwa wenyewe nafsi yake ni nguvu.

Wakati umewadia kwa wakomunist kutangaza waziwazi, mbele ya dunia nzima, maoni yao, madhumuni yao na hamu zao, kupambana na hadithi hizi za kitoto juu уa habari ya pepo wa ukomunist kwa kutoa Maelezo ya Chama chenyewe.

Kwa madhumuni hayo, wakomunist wa nchi mbalimbali wamekutanika London, na kuyatunga "Maelezo" haya yafuatayo, yachapwe kwa Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kitaliana, Kiflemish na Kidenish.

I

MABEPARI NA MAPROLETARII[2]

 

Taarikh ya ujamaa wote ulioko mpaka sasa[3] ni taarikh ya mapigano ya kitabaka.

Mwungwana na mtumwa, mtu mkubwa na mtu wa kawaida, bwana shamba na mkulima mtumwa, fundi wa ushirika wa wasanifu[4] na mwanafunzi wa kazi, kwa ufupi anayekandamiza na anayekandamizwa, walisimama kupingana daima, wakiendeleza mapigano yasiyokatizwa, mara ya siri, mara ya dhahiri, mapigano ambayo kila wakati humalizika ama kwa ujengwaji tena kwa vikubwa sana wa ujamaa, au kwa kujiteketeza wenyewe tabaka zishindanazo.

Katika zama zilizotangulia za taarikh, yakurubia kila mahali tunakuta mgawiko kamili wa ujamaa katika daraja mbalimbali, daraja za aina nyingi sana za ujamaa. Katika Urumi ya zamani tunao watukufu, wenye hadhi za wapanda farasi, watu wa kawaida na watumwa; katika zama za kati, mabwanyenye wakubwa, mabwanyenye wadogo watumikiao kupata ulinzi, mafundi wa shirika za wasanifu, wanafunzi wao wa kazi, wakulima watumwa; takriban katika daraja zote hizo, tena kuna migawiko yao wenyewe midogo midogo.

Ujamaa wa kisasa wa kibepari uliochipuka kutokana na magofu у a ujamaa wa kibwanyenye haukuondosha uadui wa kitabaka. Isipokuwa umeanzisha tabaka mpya, hali mpya za kudhulumu na aina mpya za mapigano mahali pa zile za kizamani.

Zama zetu, zama za mabepari, ingawaje, zina alama hii kubwa: zimerahisisha uadui wa kitabaka. Ujamaa mzima unazidi kugawika katika kambi mbili kubwa zinazohasimiana, katika tabaka mbili kubwa zenye kukabiliana sawasawa: mabepari na maproletarii (wafanya kazi). Kutokana na wakulima watumwa wa zama za kati walichipuka watu huru wa miji ya mwanzo. Kutokana na daraja hii ya watu wa miji chipukizi za mwanzo za ubepari zilianza kukua.

Uvumbuzi wa Amerika na wa njia ya bahari kuizunguka Afrika uliufagilia uwanja mpya ubepari unaoanza kukua. Masoko ya Bara Hindi ya Mashariki na China, kuitawala Amerika, kufanya biashara na makoloni, uongezekaji wa njia za uuzaji na ununuzi wa bidhaa kwa kawaida uliipa biashara, usafiri wa baharini na uchumi shauku isiyopata kujulikana kabla, na hivyo basi, kusababisha usitawi wa haraka wa chipukizi ya kithawra katika ujamaa wa kibwanyenye unaotota.

Utaratibu wa zamani wa kibwanyenye wa uchumi, ambao katika utaratibu huo utoaji wa uchumi ulikuwa ukihoziwa na shirika za wasanifu, sasa hautoshelezi tena matakwa yanayozidi kuwa mengi ya masoko mapya. Utaratibu wa vikao vya kutengeneza bidhaa (maiiufekcha) ulishika mahali pake. Mafundi wa shirika hizo walipigwa kumbo na tabaka ya kati ya uchumi; ugawanaji wa kazi baina ya shirika mbalimbali ulitoweka mbele ya ugawanaji wa kazi katika kila kikao kimoja cha kazi.

Wakati huu masoko yakazidi kuongezeka, matakwa yakazidi kumiminika. Hata vikao vya kutengeneza bidhaa havikuweza tena kutosheleza. Hapo tena, mitambo iendayo kwa mvuke na mashine zimefanya mageuzi makubwa katika uchumi. Mahali pa vikao vya kutengeneza bidhaa pakachukuliwa na uchumi mkubwa wa kisasa, mahali pa tabaka ya kati ya uchumi pakachukuliwa na mamilioneya wenye kuhozi uchumi, viongozi wa majeshi mazima mazima ya uchumi, mabepari wa kisasa.

Uchumi mkubwa umeanzisha soko la dunia nzima, ambalo limefunguliwa njia kwa uvumbuzi wa Amerika. Soko hili limesababisha usitawi mkubwa sana kwa biashara, usafiri wa baharini na wa nchi kavu. Usitawi huu, kwa upande wake, pia umeleta athari juu ya uongezekaji wa uchumi; na kwa kiasi kile kile sawa na cha uongezekaji wa uchumi, biashara, usafiri wa baharini, njia za reli, ndicho mabepari wa kisasa walikua, wakaongeza rasilmali yao, na kuisukuma nyuma kila tabaka iliyorithiwa kutoka zama za kati.

Tunaona, basi, jinsi mabepari wa kisasa walivyo nafsi yao ni matokeo ya maendeleo ya mwendo mrefu, ya mkururo wa mabadilisho makuu katika njia za uchumi na ubadilishanaji wa bidhaa.

Kila daraja katika maendeleo уa mabepari ilifuatwa na mafanikio kama hayo ya kisiasa yaliyofanywa na tabaka hiyo. Tabaka у a wakandamizwao chini уa utawala wa mabwanyenye, jumuiya ya silaha na yenye kujitawala wenyewe katika komyuni[5] у a zama za kati, mara hapa jamhuri huru ya kimjini (kama ilivyo katika Taliana na Ujerumani); mara kule - tabaka ya tatu ya ufalme itozeshwayo kodi ya kichwa (kama ilivyo katika Ufaransa), baadaye katika wakati wa vikao vya kutengeneza bidhaa, ikitumikia ama ufalme wenye tabia ya ubwanyenye nusu au ufalme kamili kama ndiyo kinga dhidi ya watukufu, na kwa hakika ndio msingi madhubuti wa ufalme mkubwa wo wote, na mwishowe, tangu uanzishwaji wa uchumi wa kisasa na wa soko la dunia, tabaka ya mabepari imejipatia wenyewe nguvu kamili za kisiasa katika serikali ya kisasa ya wajumbe. Serikali ya dola ya kisasa ni komiti tu kwa ajili ya kuyaendesha mambo yao mabepari wote pamoja.

Mabepari wamefanya kazi ya kithawra kabisa katika taarikh.

Mabepari po pote pale walipopata nguvu, waliyakomesha mahusiano yote ya ubwanyenye, ya kumtukuza mwanamume na mahusiano yasiyotazamia faida. Bila ya huruma wameyachopoa mbalimbali mafundo ya kila aina ya kibwanyenye yaliyomfunga mtu kwa "mabwana" zake "alioumbiwa", na hawakubakiza mahusiano yo yote mengine kati ya binadamu kwa binadamu mwenzake isipokuwa kujipendelea nafsi yake mtu tu, isipokuwa kuhesabiana kwa pesa tu. Wamezizamishilia mbali furaha kubwa za juhudi у a dini, hamu kubwa у a kupenda ushujaa, na kuvutwa na huruma zaidi kuliko busara, katika maji baridi у a kufanya mambo yatakayomletea faida mtu mwenyewe tu nafsi yake. Wameibadilisha thamani у a mtu kuwa kitu chenye thamani ya biashara tu, na mahali pa aina nyingi sana za uhuru uliotolewa na kuthibitishwa mikatabani wameanzisha uhuru huo mmoja wa aibu - uhuru wa biashara. Kwa ufupi, mahali pa unyonyaji damu, wenye kufunikwa na madanganyo ya dini na ya kisiasa, wameleta unyonyaji damu usiofunikwa na cho chote, usio na haya, usio na kificho na wa kikatili.

Mabepari wameiondolea heshima kila kazi ambayo hapo mwanzoni ilikuwa ikitukuzwa na kuheshimiwa sana. Warnewageuza matabibu, wanasheria, makasisi, washairi, wataalamu, kuwa vibarua vyao vya kuajiriwa.

Mabepari wameiondoshelea mbali sitara ya kuoneana huruma kwa watu wa nyumba moja, na kuyageuza mahusiano ya watu wa nyumbani kuwa ni mahusiano ya pesa tu.

Mabepari wamefichua jinsi ilivyokuwa kwamba uonyeshaji nguvu wa kikatili katika zama za kati, ambao wapingaji maendeleo walikuwa wakiuhusudu, ulikuwa ukipata jazua inayofalia katika ukunguni wa kivivu kabisa. Wamekuwa wa mwanzo kuonyesha nini matendo ya mtu yanaweza kuleta. Wamefanya mambo ya ajabu yapitayo kabisa majengo ya mawe ya Misri, mifireji у a maji у a Kirumi, na makanisa ya Gothic; wameifanya misafara mingine ambayo inaipita kabisa uhamaji wa mataifa na misafara ya Msalaba.[6]

Mabepari hawawezi kuishi bila ya daima kuzibadilisha vikubwa sana zana za uchumi, na kwa hivyo pia mahusiano ya uchumi, na pamoja na hayo mahusiano yote ya ujamaa. Kuhifadhi njia za kizamani za uchumi katika umbo lisilobadilishwa, kulikuwa, kinyume na hayo, ndiyo shuruti ya kwanza ya kuishi kwa tabaka zote za mwanzo za uchumi. Daima kuubadilisha vikubwa sana uchumi, kuyachafua bila ya kukatizwa mahusiano yote у a ujamaa, wasiwasi na misukosuko ya daima yanazitofautisha zama za mabepari kutokana na zile zote za kabla. Mahusiano yote yaliyowekwa imara, yaliyoganda sana, pamoja na mkururo wao wa maoni na fikira za zamani zenye kuheshimiwa yanafagiliwa, mahusiano ycte yanayozaliwa upya yanaonekana kuwa hayafai tena hata kabla hayakupata nguvti. Yote yaliyokuwa yameganda huyeyuka hewani, yote yale yaliyo matakatifu hunajisishwa, na mwanadamu mwishowe amelazimika kizikabili kwa akili yenye busara, hali zake halisi za maisha, na mahusiano yake yeye na mwenzake.

Haja ya soko likualo daima kwa ajili ya bidhaa zao inawarandisha mabepari kote duniani. Inawabidi wajipachike kila mahali, wakae kila mahali, waanzishe mahusiano kila mahali.

Mabepari kwa kulitumilia soko la dunia wamefanya utoaji na utumiaji wa bidhaa wa nchi у о yote kuwa na tabia у а kilimwengu. Kwa uchungu mkubwa wa moyo wa wapingaji maendeleo, wameuondosha chini ya miguu ya uchumi msingi wa kitaifa. Kazi zote za uchumi za kitaifa zilizowekwa zamani zimevunjwa au zinavunjwa kila siku. Zinabadilishwa kwa kazi mpya za uchumi, ambazo uanzishwaji wake unakuwa ni jambo la kufa kupona kwa mataifa yote yaliyostaarabika, kwa kazi za uchumi ambazo hazivitumii vitu visivyotengenezwa vya kienyeji, lakini vitu vilivyochukuliwa kutoka sehemu za mbali kabisa za dunia, kazi za uchumi ambazo zinatengeneza bidhaa za kiwandani ambazo butumiwa si nyumbani tu, bali katika kila pembe ya dunia. Badala ya haja za zamani kutoshelezwa na bidhaa za nyumbani, tunakuta haja mpya, zenye kutaka zitoshelezwe kwa bidhaa za mahali na nchi za mbali. Mahali pa kujitenga kizamani kwa taifa moja moja na kujitosheleza wenyewe, tuna maingiliano katika kila upande, kutegemeana kati ya mataifa ya dunia nzima. Kama ilivyo katika utengenezaji wa vitu, basi ni vivyo hivyo kwa utengenezaji wa akili. Mambo ya akili yafanywayo na taifa moja huwa ni mali ya wote. Kujifikiria kwa taifa moja na kutofikiri mataifa mengine kunazidi kuwa hakuyumkiniki, na kutokana na uandishi wa kienyeji na wa nyumbani, panazuka uandishi mpya wa dunia nzima.

Mabepari, kwa kutengeneza mbiombio zana zote za uchumi ziwe bora, kwa kurahisisha njia za usafiri, wanayavuta mataifa yote hata yale ya kishenzi kabisa, katika ustaarabu. Bei rahisi za bidhaa zake ndiyo marisasi makubwa sana, ambayo yanaiangusha chini mikuta yote ya Kichina, ambayo kwayo yanailazimisha chuki kubwa sana kwa wageni waliyo nayo washenzi kujitoa wenyewe. Wanayalazimisha mataifa yote, kwa hofu ya kufyekwa, kufuata mtindo wa kibepari wa uchumi, wanayalazimisha yaanzishe huo wauitao ustaarabu miongoni mwao, yaani, kuwa mabepari nafsi zao. Kwa maneno mengine, wanaiunda dunia kufuata fikira zao wenyewe.

Mabepari wamesababisha mashamba kutawaliwa na miji. Wameunda miji mikubwa sana, wameiongeza sana idadi ya wakazi wa miji kama ikilinganishwa na wa mashamba, na kwa hivyo basi imewaokoa sehemu kubwa ya watu kutokana na maisha ya kishamba yasiyokuwa na ustaarabu. Kama walivyoyafanya mashamba kuitegemea miji basi ndivyo vivyo hivyo walivyozifanya nchi zisizostaarabika na zilizostaarabika nusu kutegemea zile zilizostaarabika, mataifa ya kikulima kuyategemea yale ya kibepari, Mashariki kuitegemea Magharibi.

Mabepari wanazidi kuendelea kuondosha hali ya mtawanyiko wa watu, wa zana za uchumi, na wa mali. Wamewakusanya watu, wamezileta mahali pamoja zana zote za uchumi, na kuikusanya mali ndani ya mikono ya watu wachache. Mambo yaliyobidi yatokee kwa hayo ilikuwa ni uongozi mmoja mkuu wa kisiasa wa nchi nzima. Majimbo yaliyokuwa huru au yaliyoshikamana kwa ulegevu, yenye masilaha yao mbali, sheria zao, serikali na taratibu zao za mambo ya forodha, yalikusanywa pamoja kuwa taifa moja, likiwa na serikali moja, mpango moja wa sheria, maslaha ya namna moja ya kitabaka ya nchi nzima, mpaka mmoja na utaratibu mmoja tu wa forodha.

Mabepari, katika muda wa utawala wao ambao hautimii hata miaka mia, wameunda nguvu nyingi na kubwa sana za uchumi kupita vizazi vyote vilivyotangulia vikichanganywa pamoja. Kuziweka chini nguvu za maumbile, kufanya kazi kwa msaada wa mashine, kutumia madawa katika kazi za uchumi na kilimo, usafiri wa meli baharini, njia za reli, simu za waya ziendeshwazo kwa umeme, kuyasafisha mabara mazima kwa ajili у a kulima, kuifanya mito ifae kwa usafiri wa meli, umma wote wa watu wa nchi nzima nzima waliozuka kama miujiza kutoka katika ardhi - karne gani у a nyuma hata iliweza kudhani kwamba nguvu kama hizo za uchumi zilikuwa zimelala matumboni mwa kazi ya kijamaa?

Tunaona basi: zana za uchumi na za kubadilishana, ambazo mabepari wamejijenga wenyewe juu ya msingi wake, zinatokana na ujamaa wa kibwanyenye. Katika daraja fulani ya maendeleo ya zana hizi za uchumi na za kubadilishana, hali ambayo ujamaa wa kibwanyenye ulipokuwa ukitoa na kubadilishana bidhaa, mpangiko wa kibwanyenye wa kilimo na utoaji wa bidhaa, kwa ufupi, mahusiano ya kibwanyenye juu у a mali hayakuweza tena kufalia nguvu za uchumi zilizokwisha kua. Mahusiano haya yalipinga uchumi badala ya kuukuza. Yalibadilika kuwa mnyororo wake. Ilibidi uvunjiliwe mbali, na ukavunjwa.

Mahali pa mahusiano ya kibwanyenye pakachukuliwa na mashindano huru, yakifuatwa na umbo la kijamaa na la kisiasa lenye kufaa hali hiyo, na pia kwa utawala wa iktisadi na wa kisiasa wa tabaka ya mabepari.

Mwendo kama huo tunauona sasa mbele ya macho yetu. Ujamaa wa kisasa wa kibepari pamoja na mahusiano yake ya uchumi, ya kubadilishana bidhaa na ya mali, ujamaa uliofanya miujiza ya zana kubwa sana za uchumi na za kubadilishana bidhaa, ni kama mchawi aliyemfanya juju wa majuju kwa mazingaombwe yake na ambaye sasa hawezi tena kumzuia nguvu zake. Kwa miaka kadha iliyopita taarikh ya uchumi na biashara ni taarikh ya uasi wa nguvu za kisasa za uchumi kuyapinga mahusiano ya kisasa ya uchumi, kupinga mahusiano ya kumiliki mali, ambayo ndiyo mashuruti ya kuishi kwa ubepari na utawala wake. Inatosha kuitaja michafuko ya biashara tu kwamba kwa kurejea kwake kila baada ya kipindi fulani kunakutia katika msukosuko, kila mara kwa hatari zaidi, kuwepo kwa ujamaa mzima wa kibepari. Katika michafuko hii sehemu kubwa si ya bidhaa zilizopo sasa tu, bali hata sehemu ya nguvu za uchumi zilizoundwa kabla, zote zinatoswa. Katika michafuko hii huchomoka maafa ya kuambukiza, ambayo katika zama zote zilizopita yangalionekana ni muhali - maafa yenyewe ni ya kutoa bidhaa nyingi kupita mpaka. Ujamaa mara hujiona kuwa umerejeshwa katika hali ya ushenzi uliotokea ghafla; huonekana kama kwamba njaa; vita vya uteketezi vya dunia nzima vimeukatia kila njia ya kupata uhai; uchumi na biashara huonekana kama kwamba umekwisha haribiwa; na kwa nini? Kwa sababu kuna ustaarabu mwingi bila ya kiasi, kuna njia nyingi za kupata uhai bila ya kiasi, uchumi mwingi sana bila ya kiasi, biashara nyingi sana bila ya kiasi. Nguvu za uchumi zenye kuutumikia ujamaa hazifai tena kuendeleza mbele usitawi wa mahusiano ya kibepari juu ya mali; kinyume cha hayo, zimekuwa na nguvu sana kuyapita mahusiano haya, na mwishowe yanapinga maendeleo ya nguvu za uchumi, na mara tu nguvu za uchumi zinapozishinda pingu hizo, huleta mparaganyiko wa mambo katika ujamaa mzima wa kibepari na kuitia hatarini mali ya kibepari. Hali za ujamaa wa kibepari ni ndogo sana kuweza kuchukua mali waliyoifanya. Na vipi basi mabepari wanaishinda michafuko hii? Kwa upande mmoja kwa kuziharibu bila ya kutaka nguvu nyingi za uchumi; kwa upande mwingine kwa kusaka masoko mapya, na kwa kuyatumilia sana yale ya zamani. Hiyo ni kusema, kwa kufagia njia kwa ajili ya michafuko mingine mingi zaidi na ya uharibifu zaidi, na kwa kupunguza njia ambazo zinazuia michafuko.

Silaha walizotumia mabepari kuuangusha ubwanyenye sasa zinatumiliwa kuwapinga mabepari wenyewe.

Lakini mabepari si kama wamefua silaha zitakazokuja kuwaua tu; bali pia wamesababisha kuwako kwa watu watakaokuja kuzitumia silaha hizo kwa mikono yao - tabaka ya kisasa ya wafanya kazi - maproletarii.

Maproletarii, tabaka ya kisasa ya wafanya kazi, wanaoweza kuishi madhali wanapata kazi tu, na ambao wanapata kazi madhali kazi hiyo inazidisha rasilmali, tabaka hiyo inakua kwa kiasi kile kile kama cha mabepari, yaani, rasilmali. Vibarua hawa ambao lazima wajiuze nafsi zao mmoja mmoja, ni bidhaa, kama kitu cho chote chengine cha biashara, na kwa sababu hiyo hupata taabu zote za bahati nasibu zitokeazo mashindanoni, za kupanda na kushuka kwa bei ya soko.

Kwa sababu ya kutumiliwa mashini kwa wingi sana na kugawana kazi, kazi ya wafanya kazi imepoteza tabia yake mwenyewe, haina utamu wo wote kwa mfanya kazi. Anakuwa ni sehemu iliyobandikwa kwenye mashini, na ni kazi rahisi kabisa, yenye kuchosha sana, na ustadi mdogo wenye kuzoeleka kwa urahisi sana ndiyo anayotakiwa kufanya. Kwa hivyo, gharama kwa kazi anayofanya mfanya kazi ni ndogo sana, yakurubia kuwa kiasi cha kumwezesha aishi tu na kuendeleza mbele ukoo wake. Lakini bei ya bidhaa, na kwa hivyo pia bei ya kazi[7], ni sawasawa na gharama za utengenezwaji wake. Kwa kiasi hicho hicho, kwa hivyo, uchoshi wa kazi unapoongezeka, ujira unapungua. La, si hivyo tu, kwa kiasi mashine zinavyotumiwa na mgawanyo wa kazi unavyozidi, ndivyo, vivyo hivyo ukubwa wa kazi unavyozidi, ama kwa kucngezwa saa za kazi, ama kwa kuongeza ukubwa wa kazi itakiwayo katika kipindi fulani au kwa kuongeza mwendo wa mashine n.k.

Uchumi wa kisasa umekibadilisha kiwanda kidogo cha kufanyia kazi cha msanifu wa kizamani kuwa karakana kubwa sana ya tajiri wa uchumi. Umma wa wafanya kazi waliokusanyika katika karakana hiyo, hupangwa kama maaskari. Kama maaskari wa kawaida wa jeshi la uchumi huwekwa chini ya amri ya maafisa na masajini chungu nzima. Si kama wao ni watumwa wa tabaka ya mabepari na serikali ya kibepari tu, bali kila siku na kila saa wao ni watumwa kwa mashine, kwa msimamizi na juu kabisa, kwa mwenyewe bepari tajiri wa karakana. Udhalimu huo unapozidi kutangaza wazi kuwa faida ndiyo makusudio yake na ndiyo madhumuni yake, ndipo unapozidi kuonekana kuwa duni, kuchukiza, na kutilisha uchungu.

Kila ufundi ukiwa mdogo na kuhitaji nguvu chache katika kazi, kwa maneno mengine, kila uchumi wa kisasa unapozidi kukua, ndipo kazi ya wanaume inapozidi kuchukuliwa na wanawake na watoto. Tofauti za umri na kuwa mwanamume au mwanamke hazina tena maana yo yote katika ujamaa kuhusu tabaka ya wafanya kazi. Wao wote ni vyornbo vya kufanyia kazi, wanakuwa ghali au rahisi kuwatumia kwa mujibu wa umri wao na kuwa mwanamume au mwanamke.

Haujawahi kumalizika vizuri unyonyaji damu wa tajiri wa karakana kwa mfanya kazi, apatapo mshahara wake tu, mara huvamiwa na mabepari wengine, tajiri apangishaye nyumba, mwenye duka, mwekaji rahani n.k.

Pande la chini la tabaka ya kati - matajiri wadogo wa uchumi, wenye maduka madogo, na mabepari wadogo wanaotegemea faida kutoka rasilmali yao, wasanifu na wakulima - wote hawa pole pole huzama katika tabaka ya wafanya kazi, sababu moja ni kwamba kijirasilmali chao kidogo sana hakitoshi kuendesha makarakana makubwa ya uchumi wa kisasa, na huangamizwa katika mashindano yake na makepitalist wakubwa, sababu nyingine ni kwamba ujuzi wao unafanywa kuwa hauna maana kwa ajili ya njia mpya za utendaji wa kazi. Kwa hivyo basi wafanya kazi hukusanywa kutoka tabaka zote za watu wa nchini.

Tabaka ya wafanya kazi hupitia daraja mbalimbali za ukuaji wake. Inapozaliwa tu huanza mapigano yake na mabepari.

Mwanzoni mapigano hufanywa na kibarua mmoja mmoja, halafu na wafanya kazi wa kiwanda kimoja, baadaye watu wafanyao kazi у a aina moja у a uchumi katika mahali pamoja, dhidi ya bepari mmoja awanyonyaye damu moja kwa moja. Hawafanyi mashambulio yao dhidi ya hali za kibepari za uchumi tu, bali dhidi ya zana zenyewe za uchumi; huziharibu bidhaa kutoka nchi za nje ambazo hushindana na bidhaa zao, huzivunja mashine, huvitia moto viwanda, hutaka kuleta kwa nguvu hali iliyokwisha toweka ya mfanya kazi wa zama za kati.

Katika daraja hii ya ukuaji wafanya kazi bado huwa ni umma uliotawanyika nchi nzima, na uliotengana sana kwa mashindano ya kiadui kati ya wao wenyewe kwa wenyewe. Ikiwa wameungana na kuwa kama kitu kizima, haya yanakuwa hayakusababishwa na juhudi уa umoja wao wenyewe, lakini ya umoja wa mabepari, tabaka ambayo, kwa kutaka kupata madhumuni yake wenyewe ya kisiasa, inalazimika na kwa muda fulani, inaweza bado, kuwachangamua wafanya kazi wote katika mapigano. Kwa hivyo katika daraja hii, wafanya kazi hawapigani na maadui zao bali na maadui wa maadui zao, yaani mabaki ya utawala kamili wa mfalme, wenye mashamba, mabepari wasiohusika na kazi za uchumi na mabepari wadogo. Basi mwendo wote huo wa kitaarikh umekusanyika mikononi mwa mabepari; kila ushindi upatikanao hapo ni ushindi wa mabepari.

Lakini kwa ukuaji wa uchumi wafanya kazi si kama wanaongezeka kwa idadi tu; wanakusanyika katika makundi makubwa zaidi, nguvu zao zinakua, na wanazidi kuzihisi nguvu hizo. Masilaha na hali mbalimbali za maisha ya wafanya kazi wenyewe huzidi kusawazishwa, kwa kiasi kile kile kama mashine zinavyoondosha tofauti zote baina ya aina mbalimbali za kazi, na yakurubia kila mahali huyapunguza malipo kuwa katika daraja ile ile moja ya chini. Mashindano ya kiadui yaongezekayo miongoni mwa mabepari, na matokeo yake, yaani, michafuko ya biashara, huifanya mishahara ya wafanya kazi kuzidi kwenda mrama, utengenezwaji usiosita wa mashine ziwe bora zaidi, usitawi wake wa haraka zaidi, unayafanya maisha yao kuzidi kuwa mabaya; mapambano kati ya mfanya kazi mmoja mmoja na bepari mmoja mmoja huzidi kuwa na tabia ya mapambano kati ya tabaka mbili. Hapo tena wafanya kazi huanza kujichanganyisha kuunda vyama vya wafanya kazi kuwapinga mabepari; huchanganyika pamoja ili kuyahifadhi malipo yao; wanaanzisha jumuiya za daima ili kujiwekea akiba pindi ukitokea uasi. Huku na huko mapigano humalizikia katika uasi.

Mara kwa mara wafanya kazi hushinda, lakini kwa muda mchache tu. Matokeo ya kweli ya mapigano yao hayamo katika mapatikano ya papo hapo, bali katika umoja wa wafanya kazi unaozidi kukua. Umoja huu unasaidiwa kwa kutengenezwa njia bora zaidi za kufikiliana ziundwazo na uchumi wa kisasa na hayo huwawezesha wafanya kazi wakaao mahali mbalimbali kupelekeana habari. Kupelekeana habari huko ndiko kulikohitajiwa kuyaendesha kwa pamoja mapigano mengi ya mahali mbali mbali, yote yenye tabia moja, kuyafanya kuwa mapigano mamoja ya kitabaka ya nchi nzima. Lakini kila mapigano ya kitabaka ni mapigano ya kisiasa. Na umoja huo, ambao uliwachukua watu wa miji ya zama za kati, kwa njia zao mbovu, makarne mengi kuupata, wafanya kazi wa kisasa, tunashukuru kwa kuwepo njia za reli, wanaupata kwa miaka michache tu.

Huku kujipanga kwa wafanya kazi katika tabaka moja, na kwa hivyo katika chama cha kisiasa, kunaharibiwa mara kwa mara kwa mashindano ya kiadui kati ya wafanya kazi wenyewe kwa wenyewe. Lakini hunyanyuka tena na tena kuwa na nguvu zaidi, madhubuti zaidi na kukubwa zaidi. Kunalazimisha utambuzi wa masilaha fulani ya wafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kwa kuchukua fursa ya mgawanyiko ulioko kati ya mabepari wenyewe. Hivyo basi ndio ikapasishwa sheria ya kufanya kazi kutwa saa kumi katika Uingereza.

Yote kwa pamoja mapambano kati ya tabaka mbalimbali za ujamaa wa zamani yanaendeleza mbele, kwa njia nyingi, mwendo wa usitawi wa tabaka ya wafanya kazi. Mabepari wanashughulika na vita vya daima: kwanza na watu wakubwa, baadaye na makundi yale ya mabepari wenyewe ambao masilaha yao yameshakuwa yanapingana na maendeleo ya uchumi; kwa wakati wote na mabepari wa nchi za kigeni. Katika vita vyote hivi wanajiona nafsi zao wamelazimika kukimbilia kwa wafanya kazi, kuomba msaada wao, na kwa hivyo, kuwaburura katika mambo ya kisiasa. Kwa hivyo, mabepari nafsi zao, huwapa wafanya kazi chanzo cha elimu ya siasa na уa kawaida, kwa maneno mengine, wao ndio wanaowapa wafanya kazi silaha za kuja kupigana na mabepari.

Zaidi, kama tulivyokwisha ona, sehemu nzima nzima za tabaka zitawalazo, kwa sababu ya maendeleo ya uchumi, hutelemshwa chini kuwa wafanya kazi, au kwa uchache, huwamo hatarini kwa hali zao za maisha. Hawa pia huwapa wafanya kazi chanzo kipya cha elimu.

Mwishowe, katika nyakati ambapo mapigano ya kitabaka yanakurubia saa yake ya uamuzi, mwendo wa kuvunjika ufanyikanao katika tabaka ya wanaotawala, kwa hakika katika upeo wote wa ujamaa wa zamani, unakuwa na nguvu sana, mkali sana, hata sehemu ndogo ya tabaka ya wanaotawala hujigawa pande, na kuiunga tabaka ya kithawra, tabaka yenye kuzishika siku zijazo mikononi mwake. Kwa hivyo, kama ilivyokuwa zamani sehemu fulani ya watukufu walikwenda upande wa mabepari, basi ndivyo ilivyo sasa sehemu ya mabepari inakwenda upande wa wafanya kazi, na hasa, sehemu ya wataalamu wa kibepari wa mambo ya mawazo ambao wamejiinua nafsi zao kwenye daraja ya kuweza kupima kwa fikira mwendo mzima wa kitaarikh.

Katika tabaka zote zinazosimama uso kwa uso kuwapinga mabepari leo, tabaka ya maproletarii tu pekee ndiyo tabaka ya kweli ya kithawra. Tabaka nyingine zote huoza na mwishowe hutoweka kwa kupambana na uchumi wa kisasa; tabaka ya maproletarii ndiyo kizazi chake wenyewe.

Daraja ya kati ya ujamaa, yaani matajiri wa viwanda vidogo, wauza duka, wasanifu na wakulima - wote hawa hupigana na mabepari kujiokoa wasipoteze uhai wao kama ni sehemu ya daraja ya kati ya ujamaa. Kwa hivyo wao si watu wapendao mabadilisho bali ni watu wapendao kuhifadhi mambo yale yale ya kizamani. Wala si hayo tu, wao ni wapinga maendeleo, kwani wanataka kurejesha nyuma mwendo wa kitaarikh. Ikiwa kwa bahati yo yote wamekuwa wanapendelea mabadilisho, hayo ni kwa sababu ya kuwa itawabidi wawe wafanya kazi, kwa sababu hawapiganii maslaha yao ya sasa, bali maslaha yao yajayo, kwa sababu wanaacha msimamo wao wenyewe na kujiweka kwenye msimamo wa wafanya kazi.

Malofa (“ tabaka yenye hatari") watu waovu.wa ujamaa,, watu wale wanaooza kimya waliotupwa na daraja za chini kabisa za ujamaa wa zamani, wanaweza mahali fulani fulani kukumbwa katika mwendo na thawra ya maproletarii; hali zao za maisha, ingawaje, zinawatayarisha zaidi kwa kufanya kazi ya kutumiliwa kwa mrungura kutekeleza vitimbi vya kupinga maendeleo.

Katika hali za maisha za wafanya kazi, hali za maisha za ujamaa wa zamani kwa hakika zimeshazamishwa. Mfanya kazi hana mali yo yote; mahusiano yake kwa mkewe na wanawe hayafanani tena hata kidogo na yale ya mahusiano ya ukoo wa kibepari; kazi ya kisasa katika uchumi, kutawaliwa kwa sasa na rasilmali, kama ilivyo katika Uingereza basi vivyo hivyo katika Ufaransa, katika Amerika kama katika Ujerumani, kumemfutia alama zo zote za tabia ya nchi yake. Sheria, adabu, dini, kwake yeye anaona ni aina chungu nzima za maoni ya kizamani ya kibepari, ambazo nyuma yake maslaha mengi ya kibepari kama hayo yanajificha.

Tabaka zote zilizotangulia baada ya kuzikamata nguvu zote mikononi mwao zilijitahidi kuimarisha vyeo vyao walivyokwisha vipata ili kwa kuukandamiza ujamaa mzima kuhakikisha njia yao ya kushika machumo. Wafanya kazi hawawezi kuwa mabwana wa nguvu za uchumi za ujamaa, isipokuwa kwa kuondosha njia yao wenyewe ya zamani ya kushika machumo, na kwa hivyo pia kila njia nyingine ya zamani ya kushika machumo. Hawana chao cho chote cha kutaka kukipata na kukiimarisha; wajibu wao ni kuzivunjilia mbali hifadhi na dhamana zote za zamani kwa mali isiyokuwa ya wote.

Nyendo zote za kitaarikh za zamani zilikuwa ni nyendo za watu wachache tu au kwa ajili ya maslaha ya watu wachache tu. Mwendo wa wafanya kazi ni mwendo huru na wenye fahamu, wa watu wengi sana, kwa ajili ya maslaha ya watu wengi sana. Wafanya kazi, tabaka ya chini sana ya ujamaa wetu wa sasa, hawawezi kufurukuta, hawawezi kujinyanyua juu, bila ya kuzirushilia mbali daraja zote za ujamaa unaotawala.

Ingawa bado hayajawa kitu, lakini yameshaanza kuumbwa, mapigano ya wafanya kazi dhidi ya mabepari mwanzoni ni mapigano ya nchini. Wafanya kazi wa kila nchi lazima kwanza, bila ya shaka, wawafyeke mabepari wao wenyewe.

Katika kuonyesha daraja za kawaida kabisa za ukuaji wa tabaka ya wafanya kazi, tuliona vita vya nchini vilivyofichika kidogo, vifanywavyo katika ujamaa unaokuwapo, mpaka hadi ambapo vita humalizikia katika thawra waziwazi, na ambapo upinduliwaji wa mabepari kwa nguvu unaweka msingi wa kushika utawala kwa wafanya kazi.

Mpaka wakati huu wa leo, kila aina ya ujamaa imetegemezwa, kama tulivyokwisha ona, juu ya uadui kati ya tabaka zikandamizazo na zikandamizwazo. Lakini ili kuweza kuikandamiza tabaka fulani, hali fulani lazima zihakikishiwe ili kwamba katika hali hizo inaweza, angalau kuendelea na maisha yake ya kitumwa. Wakulima watumwa katika hali za utumwa wa kishamba, waliweza kujinyanyua kufikilia kupata uwanachama wa komyuni, kama mabepari wadogo walivyoweza kuwa mabepari katika utawala wa kibwanyenye kamili. Mfanya kazi wa sasa, kinyume cha hayo, badala ya kujinyanyua kwa maendeleo ya uchumi, anazama chini zaidi na zaidi kuliko hali za maisha za tabaka yake mwenyewe. Anakuwa fukara kabisa, na ufukara unakua mbio sana kuliko idadi ya watu na mali. Na hapa inakuwa wazi, kwamba mabepari hawafai tena kuwa ndiyo tabaka inayotawala katika ujamaa, wala kushurutisha hali za maisha za tabaka yake juu ya ujamaa kama ndio sheria inayotawala. Hawafai kutawala kwa sababu hawawezi kuwadhamini watumwa wao hata daraja ya maisha ya kitumwa, kwa sababu hawawezi kufanya kitu kuwazuia wasizame katika hali ambapo inawabidi wawalishe, badala ya kulishwa na wao. Ujamaa hauwezi kuishi tena chini ya utawala wa mabepari, kwa maneno mengine kuwapo kwake hakupatani tena na ujamaa.

Shuruti muhimu ya kuwapo, na utawala wa tabaka ya mabepari, ni kukusanywa rasilmali nyingi mikononi mwa watu wachache. Shuruti ya kuwapo rasilmali ni kazi iajiriwayo. Kazi iajiriwayo inaselelea moja kwa moja kwa kutegemea mashindano ya kiadui kati ya vibarua. Maendeleo ya uchumi, ambayo wakuzaji wake bila ya hiari zao ni mabepari wasiokuwa na nguvu ya kuyapinga, huubadilisha utengwaji wa wafanya kazi, kwa sababu ya mashindano ya kiadui, kwa kuwachanganyisha pamoja kithawra, kwa njia ya jumuiya. Kwa hivyo, ukuaji wa uchumi wa kisasa unavunja kutoka chini у a miguu yao misingi ile ile ambayo juu yake mabepari wanachuma na kushika machumo. Kwa hivyo, juu ya yote, hao ambao mabepari wanawazaa ni wachimba kaburi lao wenyewe. Uangukaji wake na ushindi wa maproletarii ni mambo sawa yasiyoweza kuepukika.

II

MAPROLETARII NA WAKOMUNIST

Wakomunist wana mahusiano gani na maproletarii tukiwachukulia wote pamoja?

Wakomunist si chama mbali kinachopinga vyama vingine vya tabaka ya wafanya kazi.

Hawana maslaha yaliyo mbali na yanayotengana na yale ya maproletarii wote.

Hawafanyi kanuni zo zote zao wenyewe kama za kundi mbali, ambazo kwazo wangetaka kuufinyanga na kuupa umbo mwendo wa maproletarii.

Wakomunist wanatofautika na vyama vingine vya tabaka ya maproletarii kwa mambo haya tu: 1. Katika mapigano ya maproletarii wa nchi mbalimbali, wanafahamisha na kuyaleta mbele maslaha ya pamoja ya wafanya kazi wote, bila у a kutegemea taifa lo lote. 2. Katika daraja mbalimbali za ukuaji wa mapigano ya tabaka ya maproletarii kuwapinga mabepari wao siku zote na kila mahali wanawakilisha maslaha ya mwendo mzima.

Kwa hivyo, wakomunist, kwa upande mmoja, katika matendo, wao ni sehemu iliyoendelea mbele, na shupavu kabisa ya vyama vyote vya tabaka ya wafanya kazi vya kila nchi, ile sehemu ambayo inawasukuma wengine wote wende mbele; kwa upande mwingine, kwa mujibu wa mawazo, wao wanawapita maproletarii wengine wote juu уa kufahamu vizuri njia ya mwendo huo, hali zilizopo, na matokeo ya kawaida ya mwendo wa maproletarii.

Madhumuni ya karibu zaidi ya wakomunist ni yale yale kama ya vyama vingine vyote: kuwafanya maproletarii wawe ni tabaka, kuuangamiza utawala wa mabepari, kuutia utawala wa kisiasa mikononi mwa maproletarii.

Maamuzi ya mawazo ya wakomunist, kwa hali yo yote ile hayakutegemezwa juu уa msingi wa fikira au kanuni zilizobuniwa, au kuvumbuliwa na mletaji mabadilisho madogo madogo huyu wala yule duniani.

Hayo yanaonyesha kwa juujuu tu, mahusiano halisi katika mapigano haya ya sasa ya kitabaka, katika mwendo wa kitaarikh upitao mbele ya macho yetu. Uondoshwaji wa mahusiano ya zamani ya kumiliki mali siyo kabisa alama muhimu ya ukomunist tu.

Mahusiano yote ya kumiliki mali katika siku za nyuma yamekuwa daima yakitegemea mabadiliko ya kihistoria yanayosababishwa na mabadiliko katika hali za kihistoria.

Thawra уa Ufaransa, kwa mfano, iliondoa miliki уa kibwanyenye kwa kuipendelea miliki ya kibepari.

Alama muhimu ya ukomunist siyo kuondosha mali yote, bali kuondosha mali ya kibepari.

Lakini mali ya kisasa ya kibepari isiyomilikiwa na wote ni matokezo ya mwisho na yaliyokamilia kabisa ya utaratibu wa kuchuma na kumiliki machumo, ambao umewekwa juu ya msingi wa uadui wa kitabaka, juu ya wengi kunyonywa damu na wachache.

Kwa maana hii, mawazo ya wakomunist yanaweza kufupizwa katika jumla moja tu: uondoshwaji wa mali isiyokuwa ya wote.

Sisi wakomunist tumekemewa kwa kuambiwa kuwa tuna hamu ya kutaka kuondosha haki ya mtu kuwa na mali kama ndio faida ipatikanayo kwa kijasho chake mwenyewe, mali ambayo inaambiwa kuwa ndio msingi wa uhuru wa binafsi, wa matendo na kujitegemea kwa mtu mwenyewe.

Mali iliyopatikana kwa taabu, kwa mtu mwenyewe nafsi yake, aliyoichuma mwenyewe! Je, inakusudiwa aina ya mali ya bepari mdogo na ya mkulima mwenye hali ndogo, aina ya mali iliyoitangulia ile ya kibepari? Haina haja ya aina ya mali hiyo kuondoshwa; usitawi wa uchumi umeshaiteketeza kwa wingi mkubwa, na bado unaendelea kuiteketeza kila siku.

Au inakusudiwa aina ya mali ya kisasa ya kibepari isiyokuwa у a wote?

Lakini kazi iajiriwayo inaweza kumfanyia mali yo yote mfanya kazi? Haiwezi hata chembe. Inafanya rasilmali, yaani, aina ile ya mali ambayo inaitumilia kazi iajiriwayo, mali ambayo haiwezi kuongezeka isipokuwa juu ya mashuruti ya kuzaa kazi mpya iajiriwayo kwa ajili ya kuitumilia upya. Mali, katika umbo lake la kisasa imewekwa juu ya msingi wa uadui kati ya rasilmali na kazi iajiriwayo. Na tuangalie pande zote mbili za uadui huu.

Kuwepo kwa kepitalist, maana yake - si kuwa na hali yake mwenyewe tu katika uchumi, bali ya kijamaa vile vile. Rasilmali ni chumo la pamoja, na haliwezi kuendeshwa isipokuwa kwa kitendo cha pamoja cha watu wengi wa ujamaa, na si hivyo tu, mwishowe, kwa kitendo cha pamoja cha watu wote wa ujamaa.

Kwa hivyo, rasilmali si nguvu ya mtu mmoja tu, bali ni nguvu ya kijamaa.

Kwa hivyo, wakati rasilmali itakapogeuzwa kuwa mali ya pamoja, kuwa mali у a watu wote wa ujamaa, basi hautakuwa ubadilishwaji wa mali у a mtu mmoja, реке yake, kuwa mali ya kijamaa. Ni tabia ya kijamaa tu ya mali hiyo ambayo ndiyo itakayobadilishwa. Mali inapoteza tabia yake ya kitabaka.

Sasa na tuchukue kazi iajiriwayo.

Bei ya wastani у a kazi iajiriwayo ni malipo ya chini kabisa, yaani, kiasi cha kumwezesha mtu kuishi tu, ambacho ni lazima kabisa kipatikane ili kumwezesha mfanya kazi aweze kuishi tu kama ni mfanya kazi. Kwa hivyo, anachopata mfanya kazi kama machumo ya kazi yake ni kitu kidogo tu cha kumwezesha kuendeleza maisha yake na kuzaa wengine kama yeye. Kwa hali yo yote ile sisi hatukusudii kamwe kuondosha aina hii ya kupata machumo ya kijasho cha mtu, machumo ambayo yanatumiwa kwa kuwazaa watoto, na ambayo hayabakishi ziada yo yote ya kuweza kuajiri kazi ya wengine. Yote tunayotaka kuondosha ni tabia hii mbaya ya kupata machumo, ambapo mfanya kazi anaishi kwa ajili уa kuongeza rasilmali tu, na haruhusiwi kuishi isipokuwa maslaha ya tabaka inayotawala yanapotaka aishi.

Katika ujamaa wa kibepari wafanya kazi si lo lote si cho chote isipokuwa ni njia tu ya kuzidisha ukusanyaji wa kazi. Katika ujamaa wa kikomunist ukusanyaji wa kazi ni njia tu ya kupanua, kutajirisha na kurahisisha maisha ya mfanya kazi.

Kwa hivyo, katika ujamaa wa kibepari, ya nyuma yanatawala ya sasa; katika ujamaa wa kikomunist, ya sasa yanatawala ya nyuma. Katika ujamaa wa kibepari rasilmali ni huru na ina tabia ya ubinafsi, ambapo mfanya kazi hana uhuru wo wote wala tabia ya ubinafsi.

Na uondoshwaji wa mambo kama haya unaitwa na mabepari uondoshwaji wa tabia ya ubinafsi na uhuru! Na hivyo barabara. Kwani bila ya shaka umekusudiwa uondoshwaji wa tabia ya ubinafsi ya kibepari na uhuru wa kibepari.

Uhuru, katika hali za sasa za mahusiano ya kibepari katika uchumi, unakusudiwa kufanya biashara huru, kuuza na kununua huru.

Lakini ikiwa kuuza na kununua kutapotea, kuuza na kununua huru kutapotea pia. Soga hili juu у a kuuza na kununua huru, kama maneno yote mengine "ya kihodari" ya mabepari wetu juu ya aina zote za uhuru, yana maana kuhusu uuzaji na ununuliwaji tu ambao si huru, kuhusu watu wa miji wa zama za kati waliokuwa si huru, lakini hayana maana yo yote kuhusu uondoshaji wa kikomunist wa kuuza na kununua, uondoshaji wa mahusiano у a kibepari katika uchumi na mabepari nafsi zao.

Mnatishika sana kwa kuazimia kwetu kuondosha mali isiyokuwa ya wote. Lakini katika ujamaa wenu huu wa sasa mali isiyokuwa ya wote imeshaondoshwa kwa sehemu tisa katika kumi za idadi ya watu wote; kuwepo kwake kwa wachache kunategemea moja kwa moja juu у a kutokuwepo kwake mikononi mwa hao tisa katika kila kumi. Kwa hivyo, mnatukemea kwa kuwa sisi tumeazimia kuiondosha aina ya kumiliki mali, ambayo shuruti ya lazima kwa kuwepo kwake, ni kutokuwepo mali yo yote kwa wingi mkubwa wa watu.

Kwa ufupi, mnatukemea kwa kutaka kuondosha mali yenu. Hivyo ndivyo hasa; hayo ndiyo tuliyoazimia kufanya.

Dakika ile ile ambapo kazi iajiriwayo haiwezi tena kugeuzwa kuwa rasilmali, pesa, au mapato yanayotokana na kumiliki ardhi, kwa ufupi, kuwa nguvu ya kijamaa ambayo inaweza kuhoziwa, yaani, dakika ile ile ambapo mali ya mtu реке yake haiwezi tena kugeuzwa kuwa mali ya kibepari, dakika ile ile, mnasema, nafsi ya mtu imepotea.

Kwa hivyo, mnakubali kwamba kwa "nafsi ya mtu” hamkusudii mtu ye yote mwingine isipokuwa bepari, yaani mtu mwenye kumiliki mali wa tabaka ya kibepari. Nafsi kama hiyo, hakika, lazima ifyekwe.

Ukomunist haumnyimi mtu ye yote uwezo wa kupata machumo ya ujamaa; yote unayoyafanya ni kumnyima uwezo wa kuwa shuruti sha wengine wamfanyie kazi mtu kwa sababu у a huko kumiliki kwake mali.

Umeletwa ubishi mmoja kwamba itakapoondoshwa mali isiyokuwa у a wote basi kazi zote zitasita, na uzembe utajaa dunia nzima.

Kwa mujibu wa haya, ujamaa wa kibepari zamani ungalikuwa umeshatupwa jaani kwa ajili ya uvivu mtupu; kwani wale watu wanaofanya kazi, hawapati cho chote, na wale wanaopata kitu, hawafanyi kazi. Ubishi wote huu si lo lote si cho chote bali ni maelezo mengine ya huo usemi: kwamba hapataweza tena kuwepo kazi iajiriwayo madhali hapana tena rasilmali.

Ubishi wote ulioshikilia kupinga njia za kikomunist za kutoa na kupata machumo ya vitu, kwa njia hiyo hiyo, umeshikilia kupinga njia za kikomunist za kutoa na kupata machumo ya kazi ya akili. Kama ilivyokuwa kwa mabepari, upoteaji wa mali ya kitabaka, kwao wao ni upoteaji wa uchumi nafsi yake, basi ni vivyo hivyo, upoteaji wa ustaarabu wa kitabaka kwao wao ni upoteaji wa ustaarabu wote.

Ustaarabu huo, ambao wanaulilia sana kwa kupotea kwake, kwa watu wengi sana, ni mafundisho ya kutenda kama mashine tu.

Lakini msizozane madhali mnapima uondoshaji wetu wa mali у a kibepari kwa mujibu wa kipimo chenu cha kibepari cha fikira za uhuru, ustaarabu, sheria na kadhalika. Hayo mawazo yenu yametokana na mahusiano ya kibepari katika uchumi na mahusiano ya kibepari juu ya kumiliki mali, kama zilivyokuwa haki zenu si lo lote isipokuwa ni nia ya tabaka yenu ambayo imefanywa kuwa sheria iwaambatayo wote, nia, ambayo asili yake inaamuliwa na hali za iktisadi za kuwapo kwa tabaka yenu.

Fahamu yenu mbaya ya kichoyo ambayo inakuchocheeni nyinyi kuyageuza mahusiano yenu ya uchumi na mahusiano ya kumiliki mali kutokana na mahusiano ya kihistoria ambayo huchomoza na kutoweka katika maendeleo ya uchumi, kuwa ndiyo kama sheria za milele za maumbile na za akili - fahamu hii mbaya mnayo nyie pamoja na kila tabaka iliyotawala na iliyokutangulieni. Yote myaonayo kuhusu mali ya kizamani, yote mnayokiri kuhusu mali ya kibwanyenye, bila ya shaka hamthubutu kukiri kuhusu aina yenu wenyewe ya mali ya kibepari.

Kuondoshwa ukoo! Hata wapendao mabadilisho makubwa kabisa huhamaki kwa shauri hili ovu la wakomunist.

Je, ukoo wa kisasa wa kibepari uko juu ya msingi gani? Juu ya rasilmali, juu ya kujipatia faida pekee. Katika umbo lake lililokua kamili ukoo huu upo miongoni mwa mabepari tu. Lakini hali hii ya mambo inapata jazua yake kwa kulazimika kukosa ukoo miongoni mwa wafanya kazi, na katika umalaya usio na kificho.

Ukoo wa kibepari utapotea baada ya muda fulani wakati ambapo jazua yake itaondoka, na zote mbili zitapotea pamoja na upoteaji wa rasilmali.

Mnatushtaki kwa kutaka kuzuia unyonywaji damu wa mtoto ufanywao na wazee wao? Kwa uhalifu huo tunajitokeza wazi kuwa ni wakosaji.

Lakini, mnasema, sisi tunaharibu mahusiano ya kupendeza kabisa, tunapoyabadilisha malezi ya nyumbani kwa yale ya kijamaa.

Na malezi yenu! Si vile vile ya kijamaa, na kutegemea mahusiano ya kijamaa ambayo mnaelimishia ndani yake, kwa njia za maingilio wazi au ya kificho, kwa kuitumia shule n.k.? Wakomunist hawakuvumbua uingiliaji kati wa ujamaa katika malezi; wao wanataka kuibadilisha tu tabia ya malezi, na kuyaokoa malezi kutokana na ushawishi wa tabaka inayotawala.

Hayo maneno matupu ya mabepari juu ya ukoo na malezi, juu ya mahusiano matukufu уa mzee na mtoto, yanazidi kuchukiza, wakati mahusiano ya ukoo wa wafanya kazi yanapozidi kutenganishwa mbalimbali kwa sababu ya maendeleo ya uchumi mkubwa, na watoto wao wanapobadilishwa kuwa ni vitu vya kawaida vya biashara na zana za kazi.

Lakini nyinyi wakomunist mnataka kumfanya mke awe wa wote, mabepari wote wanapiga makelele kwa pamoja.

Bepari anamwona mke wake kama ni chombo cha kawaida cha kazi tu. Anasikia kwamba vyombo vya kazi vitatumiliwa na wote, na, bila ya shaka, hawezi kuamua vyo vyote vingine isipokuwa kwamba hiyo ajali уa kutumiliwa na wote itawaangukia na wanawake vile vile.

Hatambui hata kidogo kwamba madhumuni hasa yaliyokusudiwa ni kuondoa hali ya wanawake kama ni vyombo vya kazi tu.

Kwa vyo vyote, hapana jambo linalochekesha zaidi kama uchungu wa kiadilifu walio nao mabepari wctu kwa hali hiyo ya mke kuwa wa wote, ambayo wanajidai itaanzishwa rasmi na bila ya kificho na wakomunist. Wakomunist hawana haja ya kuanzisha hali hiyo; hali hiyo imekuwapo tangu zama za kale sana.

Wakiwa hawakutosheka na kuwafanya wapendavyo wake na watoto wa kike wa wafanya kazi wao, bila ya kutaja wamalaya wa kawaida, mabepari wetu wanaona raha sana kutongozeana wake zao.

Ndoa za kibepari kwa hakika ni njia у a kumfanya mke awe wa wote, na kwa hivyo, sana sana, jambo ambalo wakomunist wanaweza kulaumiwa, kwa kutaka kulianzisha, ni ubadilishwaji wa hiyo hali ya mke kuwa wa wote iliyofichwa sasa kwa unafiki, na ihalalishwe wazi wazi. Lakini inajidhihirisha wenyewe kwamba uondoshwaji wa mahusiano ya kisasa katika uchumi lazima uje pamoja na uondoshwaji wa hali ya mke kuwa wa wote iliyochipuka kutokana na mahusiano haya, yaani, umalaya wa siri na wa dhahiri.

Wakomunist pia wanakemewa kwa kutaka kuondosha nchi ya uzalendo na utaifa.

Wafanya kazi hawana nchi ya uzalendo. Haiwezekani kuwanyang'anya kitu wasichokuwa nacho. Ilivyokuwa wafanya kazi lazima kabla ya yote wapate utawala wa kisiasa, lazima wanyanyuke kuwa ndiyo tabaka iongozayo ya taifa, lazima wao wenyewe wawe ndio taifa, mpaka sasa wao wenyewe ni wanataifa, ingawa si kwa mujibu wa maana inayokusudiwa na mabepari.

Tofauti ya kitaifa na uadui baina ya watu wa nchi mbalimbali zinazidi kutoweka siku baada ya siku, kwa sababu ya usitawi wa mabepari, ya uhuru wa biashara, ya soko la dunia, ya usawa katika njia ya uchumi na katika hali za maisha zinazofanana nayo.

Utawala wa wafanya kazi utazisababisha zipotee upesi zaidi. Juhudi za pamoja za nchi zenye kustaarabika, kwa uchache, ni moja katika mashuruti ya mwanzo kwa ajili ya ukombozi wa tabaka ya wafanya kazi.

Kwa kadiri ile ile ambayo unyonyaji damu wa mtu mmoja kwa mwingine unavyoondoshwa, basi ndivyo vivyo hivyo unyonyaji damu wa taifa moja kwa jingine utakavyoondoshwa.

Pamoja na uadui baina ya tabaka uadui wa taifa moja kwa jingine pia utaondoka.

Mashtaka yanayofanywa kutokana na maoni ya kidini, kifalsafa na kwa kawaida ya itikadi ya mawazo, kuupinga ukomunist, hayastahiki kuchunguliwa kwa makini.

Je, unatakikana ujuzi mkubwa sana ili kuweza kuelewa kwamba fikira za mtu, maoni na itikadi zake, kwa ufupi, fahamu ya mtu, inabadilika kuhusiana na kila badiliko katika hali za maisha yake ya vifaa, mahusiano yake ya kijamaa na maisha ya kijamaa?

Tarehe ya mawazo inahakikisha kitu gani kingine isipokuwa kwamba utoaji wa akili unabadilisha tabia yake kwa kulingana sawasawa na utoaji wa vifaa? Mawazo makuu ya kila zama yamekuwa siku zote ni mawazo ya tabaka yake inayotawala.

Wakati watu wanaposema juu ya mawazo yanayoufanya ujamaa kuwa ni wa kithawra, huwa wanaonyesha ukweli tu, kwamba katika ujamaa huo wa zamani, chipukizi za ujamaa mpya zimeshaanza kuota, na kwamba uondoshwaji wa mawazo у a kizamani unakwenda bega kwa bega na ugeuzwaji wa hali za kizamani za maisha.

Dunia ya kale ilipokuwa inamalizika, dini za kizamani zilizidiwa nguvu na ukiristo. Wakati mawazo ya kikiristo yalipoangushwa chini kwa mawazo у a maendeleo, ujamaa wa kibwanyenye ulikuwa ukipigana vita vya kufa kwake dhidi ya mabepari waliokuwa wakati huo wa kithawra. Mawazo ya uhuru wa dini na uhuru wa itikadi, yalikuwa yakionyesha utawala wa mashindano huru tu, katika mambo ya elimu.

"Lakini", itasemekana, "mawazo ya kidini, ya uelekevu wa moyo, ya kifalsafa, ya kisiasa na ya haki yalikuwa yakibadilishwa kwa muda wa maendeleo ya kitaarikh. Ama dini, uelekevu wa moyo, falsafa, elimu ya siasa, haki daima mambo hayo hayakupotea kwa mabadiliko haya.

"Pana, pia, mambo ya kweli ya milele, kama vile uhuru, haki, n.k. ambayo ni ya kawaida kwa daraja zote za maendeleo ya ujamaa. Lakini ukomunist unaondosha mambo yote hayo ya milele, unaondosha aina zote za dini, na uelekevu wote wa moyo, badala ya kuzisimamisha tena juu ya msingi mpya; kwa hivyo, ukomunist unakwenda kinyume na mambo yote yaliyofanyikana katika mwendo wa maendeleo ya kitaarikh ya wakati uliopita."

Mashtaka haya yanakusudia nini? Taarikh ya ujamaa wote uliopita ilikuwamo katika ukuaji wa uadui kati у a tabaka, uadui ambao ulikuwa ni wa aina mbalimbali katika zama mbalimbali.

Lakini aina у о yote uadui uliyokuwa nayo, jambo moja lilikuwapo katika zama zote za zamani, nalo ni unyonyaji damu wa sehemu moja ya watu kwa sehemu nyingine. Si ajabu, basi, kwamba fahamu ya kijamaa у a zama zote zilizopita, pamoja na aina zake nyingi na mbalimbali, inakua ndani ya namna fulani za kawaida, yaani fikira za wote, ambazo haziwezi kuondoka kabisa isipokuwa kwa utowekaji wa uadui wa kitabaka.

Thawra ya kikomunist ndiyo mfarakano mkubwa kabisa kutokana na mahusiano ya namna ya kikale ya kumiliki mali; si ajabu kwamba ukuaji wake unahusika na mfarakano mkubwa kabisa kutokana na mawazo ya kikale. Lakini na tuache ubishi wa kibepari kuupinga ukomunist.

Tumeshaona juu, kwamba hatua ya mwanzo katika thawra ifanywayo na tabaka ya wafanya kazi, ni kuwanyanyua maproletarii kuwa tabaka inayotawala, kupata demokrasi.

Maproletarii watatumia nguvu zao kubwa za kisiasa kuwapopotoa mabepari, kwa taratibu, rasilmali yote, kuziweka pamoja zana zote za uchumi mikononi mwa serikali, yaani mwa wafanya kazi waliojifanya kuwa ndiyo tabaka inayotawala, na kuongeza jumla ya nguvu za uchumi kwa upesi kama iwezekanavyo.

Bila ya shaka, mwanzoni, haya hayawezi kufanywa isipokuwa kwa njia za hatua yenye nguvu juu у a haki у a kumiliki mali na juu у a mahusiano у a kibepari katika uchumi, yaani kwa kutumia hatua, ambazo zinaonekana kwa mujibu wa iktisadi hazitoshi na hazishikiki, lakini ambazo, katika muda wa maendeleo yake, hujikunjua, hufanya zihitajie hatua nyingine zaidi kuupinga mpango wa ujamaa wa zamani na kutoepukika kuwa ndiyo njia ya kuubadilisha kabisa mtindo mzima wa uchumi.

Hatua hizi bila ya shaka zitatofautiana katika nchi mbalimbali.

Juu ya hivyo katika nchi zilizoko mbele kabisa hatua hizi zifuatazo kwa kawaida zaweza kutendeka:

1. Uondoshwaji wa kumiliki ardhi na kutumia kodi zote za kiwanja kulipia gharama za serikali.

2. Kodi у a juu yenye daraja ya pato.

3. Uondoshwaji wa haki zote za kurithi.

4. Kufilisi mali ya wageni na maharamia wote.

5. Mikopesho ya fedha kuiweka mahali pamoja mikononi mwa serikali, kwa njia za benki ya nchini yenye rasilmali ya kiserikali na kuhoziwa na serikali реке yake.

6. Kuziweka njia zote za usafirishaji mahali pamoja mikononi mwa serikali.

7. Kuongeza idadi ya viwanda na zana za uchumi zinazomilikiwa na serikali; kufyeka ardhi, na kuutengeneza vyema udongo kwa mujibu wa mpango wa pamoja.

8. Watu wote lazima wafanye kazi; uanzishwaji wa majeshi ya kufanya kazi, hasa kwa ajili ya kilimo.

9. Uchanganyishwaji wa kilimo pamoja na uchumi kuondosha taratibu tofauti zote zilizopo kati ya mji na shamba, kwa njia ya kuwagawanya watu sawa sawa katika nchi nzima.

10. Elimu ya kijamaa na ya bure kwa watoto wote. Uondoshwaji wa aina ya sasa ya kuwafanyisha kazi watoto katika viwanda. Uchanganyishwaji wa elimu pamoja na utoaji wa vifaa, n.k.

Wakati, katika mwendo wa usitawi, tofauti za kitabaka zitakapokuwa zimeshatoweka, na uchumi wote umekusanywa mikononi mwa ushirika mkubwa wa taifa zima, utawala wa kiserikali utapoteza tabia yake ya kisiasa. Huo unaoitwa kwa barabara utawala wa kisiasa, ni utawala uliodhibitiwa na tabaka moja kwa ajili у a kuikandamiza nyingine. Ikiwa wafanya kazi yaani maproletarii wakati wa mapigano yao dhidi ya mabepari, inawabidi, kwa kulazimishwa na hali ya mambo, kujikusanya pamoja kama tabaka moja, ikiwa, kwa njia ya thawra, wanajifanya kuwa ndiyo tabaka inayotawala, na kwa hivyo, kuyafyeka kwa nguvu mahusiano ya kizamani ya uchumi, basi kwa hivyo pamoja na mahusiano hayo, watakuwa wameshaondosha hali za kuwepo kwa uadui wa kitabaka na, kwa kawaida, kuwepo kwa tabaka mbalimbali, na kwa hivyo itakuwa imeshaondosha utawala wa tabaka yao wenyewe.

Mahali pa ujamaa wa kizamani wa kibepari, wenye tabaka mbalimbali na uadui wa kitabaka, tutakuwa na ushirika, ambao ndani yake usitawi huru wa kila mmoja utakuwa ndiyo shuruti ya usitawi huru wa wote.

III

MAANDISHI YA KISOSHIALIST NA YA KIKOMUNIST

1.  USOSHIALIST UPINGAO MAENDELEO

a. USOSHIALIST WA KIBWANYENYE

Kwa mujibu wa hali yao ya kihistoria, imekuwa ni kazi kubwa sana ya watu wakubwa wa Ufaransa na Uingereza kuandika vijitabu kuupinga ujamaa wa kisasa wa kibepari. Katika thawra ya Ufaransa, ya Julai mwaka 1830, na katika uchochezi wa kutaka mabadilisho ya palamenti uliofanywa Uingereza, watu hawa wakubwa walishindwa tena na kizushi hiki kichukivu. Tangu wakati huo, mapigano ya kisiasa ya kwelikweli yalikuwa kabisa hayawezekani. Vita vya maandishi tu pekee ndivyo vilivyoachiwa kufanyika. Lakini hata katika mambo ya maandishi imekuwa ni muhali kuyatumia maneno ya kizamani ya wakati wa kurejesha hali ya zamani.[8]

Ili waweze kupata huruma, watu wakubwa walilazimika kujidai kwamba wameyaacha maslaha yao wenyewe, na kufanya mashtaka dhidi ya mabepari kwa maslaha ya tabaka inyonywayo damu tu реке yake. Hivyo basi watu wakubwa walilipizia kisasi kwa njia ya kuwaimba mabwana zao wapya mashairi ya kukashifu, na kuwanong'oneza masikioni ubashiri wa kisirani kwa maafa yajayo.

Kwa njia hii ndio ukaja usoshialist wa kibwanyenye: nusu malalamiko, nusu ukashifu; nusu sauti ya wakati uliopita, nusu kutishia juu ya mambo yajayo; katika baadhi ya nyakati huwachoma mabepari moyoni kwa lawama zao kali, zenye ujanja na za nguvu; lakini siku zote athari yake inakuwa ya kuchekesha kwa kutoweza kabisa kufahamu mwendo wa historia ya kisasa.

Ili waweze kuukusanya umma wa watu kuwafuata wao, watu wakubwa huvinyanyua mbele vikapu vya wafanya kazi vya kuombea sadaka kama ndio bendera yao ya mapigano. Lakini watu, mara nyingi sana wanapoungana nao, huona nyuma yao alama za kibwanyenye za kizamani, na huwakimbia kwa kicheko kikubwa na cha utovu wa heshima.

Sehemu moja ya Legitimist[9] wa Kifaransa na "Uingereza Changa"[10] walishiriki katika mambo haya ya kuchekesha.

Katika kuelezea kwamba unyonyaji damu wao ni tofauti na ule wa mabepari, mabwanyenye husahau kwamba walinyonya damu katika hali na mambo ambayo yalikuwa ni tofauti kabisa, na ambayo sasa hayafai tena. Katika kuonyesha kwamba chini ya utawala wao wafanya kazi wa aina ya kisasa hawakuwepo, husahau kwamba mabepari wa kisasa ndio kizazi cha lazima kitokanacho na utaratibu wao wa ujamaa.

Juu ya hivyo, walificha kidogo sana tabia ya kupinga maendeleo ya utoaji makosa wao hata mashtaka yao makubwa dhidi ya mabepari hujumlika kuwa ni hivi, kwamba katika utawala wa mabepari hukuzwa tabaka, ambayo mwishowe itauripua hewani utaratibu wa kizamani wa ujamaa.

Jambo wanalowagombezea mabepari si kwa kuwa wao wanasababisha kuwapo kwa wafanya kazi wa kawaida, bali sana kwa kuwepo wafanya kazi wa kithawra.

Kwa hivyo katika matendo ya kisiasa, wao huingia katika mambo yote ya kutumia nguvu kuwapinga wafanya kazi; na katika maisha ya kawaida, bila ya kujali majigambo yao matamu, husimama kuokota matunda ya dhahabu yaangushwayo kutoka kwenye mti wa uchumi, na kuubadilisha ukweli, mapenzi na heshima kwa faida ya biashara ya sufi. viazi vya sukari, na ulevi wa mbatata.[11]

Kama kasisi alivyokwenda mkono kwa mkono na bwanyenye, ndivyo usoshialist wa kidini unavyokwenda na usoshialist wa ubwanyenye.

Hapana jambo rahisi kama kuuremba utawa wa ukiristo kwa rangi ya usoshialist. Je, ukiristo haukupaza sauti yake kupinga mali isiyokuwa ya wote, kupinga ndoa, kupinga serikali? Je, haikuhubiri badala ya haya, sadaka na umasikini, ujane na utawa, maisha ya kanisani na ukuhani? Usoshialist wa kikiristo ni maji matakatifu tu ambayo kwayo kasisi unaubariki uchungu wa moyoni wa watu wakubwa.

b. USOSHIALIST WA MABEPARI WADOGO

Watu wakubwa wa kibwanyenye hawakuwa ndio tabaka pekee iliyoteketezwa na mabepari, siyo tabaka moja tu ambayo hali zake za maisha ziliharibika na kupotea hewani mwa ujamaa wa kisasa wa kibepari. Watu wa miji na wakulima wenye mali ndogo katika zama za kati walikuwa ndio watangulizi wa mabepari wa kisasa. Katika nchi zile ambazo hazikusitawi sana kwa uchumi na biashara, tabaka hii bado huendelea kumea pamoja na mabepari wainukao.

Katika nchi ambazo ustaarabu wa kisasa umesitawishwa sana, imetokea sehemu mpya ya mabepari wadogo, wakiyumbayumba baina ya wafanya kazi na mabepari na maisha hujitokeza tena kama ni sehemu ya nyongeza kwa ujamaa wa kibepari. Lakini, mtu mmoja mmoja aliyemo katika tabaka hii, mara kwa mara hutokomezwa katika tabaka ya wafanya kazi kwa nguvu ya mashindano ya kiadui, na unavyokuwa uchumi wa kisasa unasitawi, hata wanaiona dakika ikikurubia ambapo wao watatoweka kabisa kama ni sehemu huru ya ujamaa wa kisasa, na mahali pao katika uchumi, kilimo na biashara patashikwa na wasimamizi na manokoa.

Katika nchi kama Ufaransa, ambako wakulima ni wengi zaidi kuliko nusu ya watu wote, haistaajabiwi kwamba wametokea waandishi walioko upande wa wafanya kazi kuwapinga mabepari, ambao katika kuukcsoa utaratibu wa kibepari wanatumia kipimo cha wakulima na mabepari wadogo, na kuyahifadhi mapigano ya wafanya kazi wakiwa juu ya msimamo wa maoni ya tabaka hii ya mabepari wadogo. Hivyo basi ndivyo ulivyoanza usoshialist wa mabepari wadogo. Sismondi[12] alikuwa ndiye kiongozi wa maandishi ya aina hiyo si katika Ufaransa tu, bali hata Uingereza.

Aina hii ya usoshialist imeona vizuri tofauti zilizopo katika mahusiano ya uchumi wa kisasa. Imefichua wazi udhuru wa kinafiki wa mabingwa wa iktisadi. Imehakikisha, bila ya mbishano, madhara yenye hatari yaletwayo na utendaji wa bidhaa kwa mashine na ugawanaji wa kazi; ukusanyaji wa rasilmali na ardhi mikononi mwa watu wachache; kutoa bidhaa kupindukia mpaka na michafuko; imeonyesha wazi uteketezwaji usiokimbilika wa tabaka ya mabepari wadogo na wakulima, mashaka ya wafanya kazi, mparaganyiko katika uchumi, hali ya kutokuwa sawa inayotilisha uchungu sana katika ugawanaji wa mali, vita vya uchumi vya kuteketezana baina ya mataifa, uondoshwaji wa mila za kizamani za uelekevu wa moyo, wa mahusiano ya kizamani ya watu wa nyumba moja, wa mataifa уa kizamani.

Lakini katika makusudio yake mema, aina hii ya usoshialist inapigania ama kuzirejeza tena njia za kizamani za uchumi na za biashara, na pamoja nazo pia mahusiano уa kizamani ya kumiliki mali, na ujamaa wa kizamani, au kuzishindilia kwa nguvu njia za kisasa za uchumi na biashara kuwamo ndani ya umbo la mahusiano ya kizamani ya kumiliki mali ambayo yamebomolewa nao na hayakuwa na budi kubomolewa. Katika hali yo yote mojawapo ya hizo mbili, aina hii inapinga maendeleo na pia ni ya ndotoni tu.

Maneno yake ya mwishoni: shirika za kutengeneza bidhaa na ukulima wa kizamani.

Mwishowe, wakati ambapo mambo yasiyokanushika ya kihistoria yatakapoondosha athari zote za kitendo kizuri sana cha kujidanganya wenyewe, aina hii ya usoshialist iliishia kupata desturi mbaya ya kunung'unika.

c. USOSHIALIST WA KIJERUMANI AU "WA KWELI”

Maandishi ya kisoshialist na ya kikomunist ya Ufaransa, maandishi ambayo asili yake yametokana na mkandamizo wa mabepari waliokuwa wakitawala, na hayo yalikuwa ni maonyo ya mapigano dhidi ya utawala huo, yalipelekwa huko Ujerumani katika wakati ambapo mabepari wa nchi hiyo ndiyo kwanza waanze mapigano na ubwanyenye mtupu.

Mabingwa wa elimu у a falsafa wa Kijerumani, mabingwa wasiokamilia wa elimu ya falsafa na wanaopenda maneno mazuri, kwa hamu sana waliyanyakua maandishi haya, wakisahau kabisa, kwamba maandishi haya yaliingizwa kutoka Ufaransa kupelekwa Ujerumani, ambapo hali za kijamaa za Ufaransa hazikuhama kufuatana nayo. Katika hali za kijamaa za Ujerumani maandishi haya yalikuwa hayana umuhimu wa matendo ya papo, na yakawa ni mambo yanayohusika na uandishi tu. Hivyo basi, kwa mabingwa wa Kijerumani wa elimu ya falsafa wa karne ya 18, madai ya Thawra ya mwanzo ya Ufaransa hayakuzidi cho chote isipokuwa ni madai ya "akili ya matendo" kwa wote, na utamkwaji wa nia ya mabepari wa kithawra wa Kifaransa ulionyesha machoni pao kama sheria za nia safi, nia kama ilivyolazimika kuwa, nia ya kweli ya binadamu wote.

Kazi yote ya waandishi wa Kijerumani ilikuwa ni kuleta fikira mpya za Kifaransa zije kupatana na fahamu yao ya kifalsafa ya kizamani, au hasa, kuzifahamu fikira za Kifaransa bila ya kuuacha msimamo wa maoni yao wenyewe ya kifalsafa.

Kufahamu huku kulitokea kwa njia ile ile kama lugha ya kigeni inavyosarifiwa, yaani, kwa kufasiri. Inajulikana sana jinsi makuhani walivyoaridika maisha ya kipumbavu ya mawalii wa kikatoliki juu ya maandiko ambayo yameandikwa maandishi ya fasaha ya kutoamini dini ya zama za kutambikia mizimu. Waandishi wa Kijerumani waliugeuza kinyume nyume mwendo huu kwa kuleta maandishi ya kikafiri ya Kifaransa. Waliandika upumbavu wao wa falsafa chini ya maandishi ya kiasili ya Kifaransa. Kwa mfano chini ya ukosoaji wa Kifaransa wa mahusiano у a fedha wameandika "Mfarakisho wa Utii', na chini ya ukosoaji wa Kifaransa wa serikali ya kibepari wameandika "Kuuzuliwa kwa Fungu la Wote", na vivyo hivyo.

Uanzishwaji wa mafungu haya ya maneno ya kifalsafa nyuma ya fikira ya Kifaransa waliubandika majina ya "Falsafa ya Matendo", "Usoshialist wa Kweli", "Elimu ya Kijerumani ya Usoshialist", "Msingi wa Kifalsafa wa Usoshialist", na vivyo hivyo.

Kwa hivyo, maandishi ya kisoshialist na ya kikomunist ya Kifaransa yaliondoshewa kabisa maana yake kuu. Na tangu yalivyokoma mikononi mwa Mjerumani kuonyesha mapigano ya tabaka moja dhidi ya tabaka nyingine, aliamini kwamba yeye yuko juu ya "tabia ya Kifaransa ya kujifikiria upande mmoja tu", kwamba anawakilisha siyo mahitajio у a kweli, bali mahitajio ya ukweli; si masilaha ya wafanya kazi, bali masilaha ya tabia ya kiutu, ya watu wote, wasiokuwamo katika tabaka yo yote, watu wasiokuwa wa kweli, ambao wamo katika maruirui ya ndoto za kifalsafa.

Usoshialist huu wa Kijerumani ambao uliyachukua matendo yake ya kitoto bila ya mzaha na kwa unyenyekevu, na kuyanadia kwa njia у a kelele kubwa, punde ukaanza taratibu kupoteza tabia yake ya kutokuwa na makosa kwa kushikilia kufuata kanuni tu.

Mapigano ya mabepari wa Kijerumani na hasa wa Prussia, kuwapinga mabwanyenye na utawala kamili wa mfalme, kwa maneno mengine, mwendo wa liberal, ukaanza kuwa madhubuti zaidi.

Kwa hivyo, usoshialist "wa kweli" ulipewa fursa iliyokuwa ikitamaniwa sana ya kuzikabili nyendo za kisiasa kwa madai ya kisoshialist, kama kawaida kuyalaani mawazo ya liberal, serikali yenye wajumbe wanaochaguliwa, mashindano ya kiadui ya kibepari, uhuru wa kibepari wa kupiga chapa, haki ya kibepari, uhuru na usawa wa kibepari, na fursa ya kuwahubiria watu kwamba hawana cho chote cha faida watakachopata, isipokuwa wanaweza kupoteza vyote walivyo navyo, katika nyendo hizi za kibepari. Usoshialist wa Kijerumani ulisahau, katika wakati wa haja, kwamba utoaji makosa wa Kifaransa, ambao usoshialist huo ulikuwa ndio mwangwe wake mdogo tu, ulidhania juu ya kuwepo kwa ujamaa wa kisasa wa kibepari, pamoja na hali zake za maisha zifaazo na katiba ya kisiasa ifaayo iliyopitishwa hapo, yaani mambo yale yale ambayo kupatikana kwake kulikuwa ndio makusudio ya mapigano yajayo katika Ujerumani.

Kwa serikali kamili za Ujerumani, pamoja na mkururo wake wa makasisi, walimu, mabwana shamba na makarani wasiokuwa na moyo, usoshialist huo ulitumika kama kitisho kinachofaa kuwapinga mabepari waletao hatari.

Ulikuwa ni nyongeza tamu kidogo kwa uchungu wa kupigwa viboko na risasi ambazo serikali hizi hizi zilizitumia, wakati ule ule, kuwakandamiza wafanya kazi wainukao.

Kwa hivyo, wakati usoshialist huu "wa kweli" ulivyokuwa unazitumikia serikali kama silaha ya kupigana na mabepari wa Kijerumani, pia vivyo hivyo, uliwakilisha maslaha ya wapinga maendeleo, ya mabepari wadogo wa Kijerumani. Katika Ujerumani tabaka ya mabepari wadogo, iliyorithiwa kutoka kame ya kumi na sita na tangu wakati huo ilikuwa daima ikichomoza tena katika aina mbali mbali, ndiyo msingi wa kweli wa kijamaa wa hali ya mambo iliyopo sasa.

Kuibakiza tabaka hii maana yake ni kuibakiza hali ya mambo iliyoko sasa katika Ujerumani. Kutoka utawala wa uchumi na wa kisiasa wa mabepari, mabepari wadogo wanangojea hatari ya kuangamizwa, kwa upande mmoja kwa sababu ya mkusanyiko wa rasilmali, kwa upande mwingine kwa sababu ya ukuaji wa wafanya kazi wa kithawra. Usoshialist "wa kweli" ulitokea kwao kuwaua ndege hao wawili kwa jiwe moja. Na usoshialist "wa kweli" ulitapakaa kama ugonjwa wa kuambukiza.

Juba la uzushi lililoshonewa kwa utando wa mawazo, likafumiwa maua ya maneno matamu yenye rangi za kupendeza, likachovywa katika machozi у a matamanio dhaifu, juba hili ambalo wasoshialist wa Kijerumani walilitumia kufutikia "fikira zao mbili za ukweli za milele", liliongeza uuzaji wa bidhaa yao miongoni mwa watu kama hao.

Na kwa upande wake, usoshialist wa Kijerumani ulizidi kuutambua wajibu wake kama ni msemeaji mkubwa wa mabepari wadogo wapingao maendeleo. Ulilitangaza taifa la Kijerumani kuwa ni mfano wa taifa jema, na mabepari wadogo wapingao maendeleo wa Kijerumani kuwa ni mfano wa binadamu mwema. Ulitoa tafsiri iliyofichika na yenye maana tukufu ya kisoshialist kwa kila tendo lake baya kabisa, tafsiri ambayo ndiyo kinyume kabisa cha tabia yake ya kweli. Umekwenda mbali sana hata kufika hadi ya kuupinga moja kwa moja mtindo wa ukomunist "wenye uharibifu wa kikatili", na kutangaza kwamba tabia yake kuu ya kutopendelea upande wo wote, iko juu ya mapigano yo yote ya kitabaka. Vitabu vyote, isipokuwa vichache tu visomwavyo sasa katika Ujerumani kama vile maandishi ya kisoshialist na ya kikomunist vimejaa maandishi haya machafu na dhaifu.[13]

2. USOSHIALIST WENYE KUHIFADHI YA ZAMANI AU WA KIBEPARI

Sehemu moja ya mabepari ina hamu ya kutengeneza maafa у a kijamaa, ili waweze kupata kuwepo daima kwa ujamaa wa kibepari.

Katika sehemu hii wamo mabingwa wa iktisadi, wapendao kuwafanyia watu hisani, wateteaji wa hisi za kiutu, wanaozungumza sana juu ya utengenezaji wa hali za watu wafanyao kazi, wakusanyaji wa sadaka, wanachama wa vyama vya kuzuia wanyama wasifanyiwe ukatili, wazushi wa jumuiya za kujinyima ulevi, wabadilishaji wa mambo madogo madogo wa kila aina inayoweza kufikiriwa. Aina hii у a usoshialist hata imekuwa inapangwa kuwa utaratibu kamili.

Tunaweza kukitaja kitabu cha Proudhon[14] kiitwacho Falsafa ya Uiukara kama ni mfano wa aina hii.

Mabepari wa kisoshialist wanataka hali za ujamaa wa kisasa zisiharibiwe na bila ya kufanywa mapigano na hatari zinazokuwa lazima zipatikane nazo. Wanataka kuuhifadhi ujamaa wa kisasa lakini bila ya kuwemo chipukizi zake za kithawra na zenye kuutengua. Wanataka waweko mabepari bila ya kuwepo wafanya kazi. Mabepari bila ya shaka wanaiona dunia ambayo wao ni wakubwa sana kuwa ndiyo bora kabisa; na usoshialist wa kibepari unakuza fikira hii tamu kuwa utaratibu kamili. Kwa kuwataka wafanya kazi wautekeleze utaratibu kama huo na kwa hivyo kwenda moja kwa moja kwenye Pepo Mpya ya kijamaa inahitaji kwa hakika, kwamba wafanya kazi lazima waselelee mipakani mwa ujamaa uliopo, lakini wayatupilie mbali mawazo yao yote ya chuki kuhusu mabepari.

Aina ya pili ya usoshialist huu inayotendekana zaidi, lakini haikupangika vizuri zaidi inataka kuziumbua kila nyendo za kithawra machoni pa wafanya kazi, kwa kuonyesha kuwa siyo mabadilisho haya au yale ya kisiasa, lakini mabadilisho ya hali za vifaa vya maisha, ya mahusiano ya iktisadi, ndiyo yatakayokuwa na faida kwao. Lakini kwa haya mabadilisho ya hali za vifaa vya maisha, aina hii ya usoshialist haifahamu kwa hali yo yote ile uondoshwaji wa mahusiano ya kibepari kwa uchumi, uondoshwaji ambao hauwezi kufanywa isipokuwa kwa njia ya thawra, lakini wao wanakusudia njia za kuleta mabadilisho madogo madogo yafanywayo na serikali, zenye kutegemea msingi wa kuendelea kuwepo mahusiano haya ya uchumi; kwa hivyo, ni mabadilisho ambayo kwa hali yo yote ile hayabadili hata kidogo mahusiano baina ya rasilmali na kazi iajiriwayo, na labda kwa vyo vyote vile yanapunguza gharama ya mabepari, na kurahisisha kazi ya kuendesha serikali ya kibepari.

Usoshialist wa kibepari unajitokeza sana wakati ule, na ndio wakati ule tu, unapokuwa ni aina ya fungu la maneno matupu tu.

Biashara huru! kwa faida ya tabaka ya wafanya kazi; ushuru wa kujilinda! kwa faida ya tabaka ya wafanya kazi; magereza ya upweke! kwa faida ya tabaka у a wafanya kazi - hili ndilo neno la mwisho na ndilo neno ambalo usoshialist wa kibepari unalikusudia bila ya mzaha.

Usoshialist wa mabepari unafupizwa kwa jumla moja: bepari ni bepari kwa ajili ya faida ya tabaka ya wafanya kazi.

3. USOSHIALIST NA UKOMUNIST WA NDOTONI WENYE KUKOSOA

Hatukusudii kusema hapa juu уa yale maandishi ambayo, katika kila thawra kuu ya kisasa, yameonyesha madai ya wafanya kazi, kama maandishi ya Babeuf[15] na wengineo.

Majaribio ya mwanzo ya wafanya kazi kwa ajili ya kutekeleza moja kwa moja maslaha yao wenyewe ya kitabaka, yaliyofanywa katika wakati wa kichocho cha kuenea pote, wakati ujamaa wa kibwanyenye ulipokuwa ukipinduliwa, majaribio haya yalibidi yashindwe, kwa sababu ya hali ya nyuma waliyokuwa nayo wafanya kazi wakati huo, na pia ukosekano wa hali za iktisadi kwa ajili ya ukombozi wake, hali ambazo huwa ni matokeo ya zama za kibepari tu. Maandishi ya kithawra yaliyofuata nyendo hizi za mwanzo za wafanya kazi yalibidi yawe na tabia ya kupinga maendeleo. Yalifundisha watu wote wawe watawa kwa kujinyima matamanio ya nafsi na kuulaza ujamaa katika usawa wa namna mbaya kabisa.

Taratibu za usoshialist na ukomunist ndivyo barabara zilivyokuwa zikiitwa, zile za St. Simon, Fourier, Owen[16] na wengine, zimechomoza katika uhai katika muda wa mwanzo usiositawi wa mapigano baina ya wafanya kazi na mabepari (angalia Sehemu"Mabepari na Maproletarii").

Wavumbuzi wa taratibu hizi, hakika, wanauona uadui kati ya tabaka mbalimbali, na pia tendo la chipukizi za uvunjaji ndani уa ujamaa wenyewe unaokuwapo wakati huo. Lakini kwa upande wa wafanya kazi, hawaoni hamu ya kuanzisha jambo lo lote jipya la kihistoria au kuwa na nyendo za kisiasa za реке yao.

Kama ilivyokuwa ukuaji wa uadui kati ya tabaka mbalimbali unakwenda mguu kwa mguu na usitawi wa uchumi, ndivyo vivyo hivyo ilivyokuwa hawawezi kutafuta hali za iktisadi zifaazo kwa ajili ya ukombozi wa wafanya kazi. Kwa hivyo hutafuta elimu mpya ya kijamaa, sheria mpya za ujamaa, ambazo zitaunda hali hizo.

Tendo lao wenyewe la kuvumbua halikuwa na budi lichukue mahali pa tendo la kijamaa, hali zifanyikazo mawazoni tu - mahali pa hali za ukombozi zilizoundwa na historia, upangikaji wa ujamaa uliotengenezwa kwa mujibu wa mashauri ya wavumbuzi hawa - mahali pa ukusanyaji wa wafanya kazi, unaoendelea mbele taratibu, kuwafanya kama tabaka. Historia ya wakati ujao уa dunia nzima, kwa fikira zao, itakuwa ni uenezaji na utekelezaji wa mipango yao ya ujamaa kwa matendo.

Wakati wafanyapo mipango yao, wao wana fahamu у a kushughulikia sana masilaha ya wafanya kazi, kama ndio watu wanaoteseka sana. Kwa maoni hayo, wafanya kazi wamekuja duniani kama tabaka tu inayoteswa zaidi kuliko wengine.

Lakini hali ya nyuma ya mapigano ya kitabaka, na pia mahali pao wenyewe katika ujamaa zinawafanya wasoshialist wa aina hii kujiona nafsi zao kuwa wako juu kupita uadui huo ulioko baina ya tabaka mbalimbali. Wanataka kutengeneza hali za kila mtu katika ujamaa, hata wale waliobahatika. Kwa hivyo huwanasihi watu wote, bila ya mpembuo wa tabaka; si hivyo tu, kwa kupendelea zaidi tabaka inayotawala. Kwa maoni yao, watu wakishaufahamu utaratibu wao, inatosha kuwawezesha kuona kwamba mpango wao ndio bora kabisa wa ujamaa bora kabisa uyumkinikao.

Kwa hivyo, wanakataa tendo lo lote la kisiasa na hasa la kithawra; wanataka kufikilia malengo yao kwa njia za salama, na kujitahidi kwa kufanya majaribio madogo madogo, ambayo lazima yatakuwa na ajali ya kushindwa, na kwa nguvu ya kuonyesha mfano, wafagie njia kwa mafundisho mapya ya ujamaa.

Sura kama hizo za mawazoni tu za ujamaa ujao, zilipatikana katika wakati ambapo wafanya kazi bado ni wachanga na wana fikira zifanyikazo mawazoni tu juu у a hali yao, sura hizi zinapatikana kutokana na matamanio ya moyoni ya tabaka hiyo kwa kuujenga tena ujamaa wote.

Lakini maandishi haya ya kisoshialist na ya kikomunist pia yana chipukizi za utoaji makosa. Zinaihujumu kila nguzo ya ujamaa uliopo. Kwa hivyo, wanayo mambo tele yenye thamani kwa kuwaongoa wafanya kazi. Mambo yanayofaa kutendwa yalishauriwa ndani yake - kama vile uondoshwaji wa tofauti kati ya mji na shamba, wa ukoo, wa kufanywa uchumi kwa ajili ya faida ya mtu mmoja mmoja, wa kazi iajiriwayo, tangazo la mapatano miongoni mwa watu wote, kuzigeuza kazi za serikali kuwa ni kazi za kusimamia uchumi tu - mashauri haya yote yameelekea yanaonyesha haja ya kuondosha uadui kati ya tabaka mbalimbali ambao ulikuwa wakati ule ndio kwanza unaanza kuchomoza, na watungaji wa maandishi haya waliutambua kwa umbo lake la mwanzo kabisa tu lisilokuwa wazi na lisilofafanuliwa. Mashauri haya kwa hivyo ni ya aina ya ndotoni tu.

Umuhimu wa usoshialist na ukomunist wa ndotoni wenye kukosoa una mahusiano ya kinyume kabisa kwa usitawi wa kihistoria. Kama yanavyokua mapigano ya kitabaka na kuwa na umbo maalum, hiyo hamu ya kuchekesha ya kusimama juu ya mapigano haya, haya mashambulio ya kuchekesha, hupoteza thamani yake yote ya matendo na uhalalishaji wa akilini. Kwa hivyo, ingawa waanzilishi wa taratibu hizi walikuwa kwa hali nyingi ni watu wapendao mabadilisho makubwa, wafuasi wao, katika kila hali, walifanya madhehebu yanayopinga maendeleo. Wanang'ang'ania kwa nguvu maoni ya zamani ya walimu wao, bila ya kufikiri usitawi wa kihistoria wa maendeleo ya wafanya kazi. Kwa hivyo, wao wanajaribu, na hufanya mara kwa mara, kuyadhoofisha mapigano ya kitabaka na kuupatanisha uadui ulioko kati ya tabaka mbalimbali. Bado wanaota juu ya kufuzu, kwa njia ya majaribio, taratibu zao za usoshialist wa ndotoni wa ujamaa, juu ya kuzigundua phalansteres" moja moja, juu ya kuanzisha makoloni ya nyumbani ("Home-colonies” ), juu ya kuanzisha "Kiikaria Kidogo"[17] - vijuzuu vya Pepo Mpya - na ili kuweza kutimiliza hizo ndoto zao, inawabidi wavute hisi na pesa za mabepari. Pole pole huzama chini kuwa katika fungu la wasoshialist wapingao maendeleo na wenye kuhifadhi ya zamani walioonyeshwa hapo juu, wakitofautiana nao kwa kushikilia kwa mpango kutumia kanuni tu bila ya kutumia akili, na kwa imani yao ya kishupavu juu ya nguvu ya ajabu ya elimu yao ya kijamaa.

Kwa hivyo, wao kwa nguvu hupinga matendo yote ya kisiasa kwa upande wa wafanya kazi; matendo kama hayo, kwa mujibu wa mawazo yao, yanaweza kusababishwa na kutoamini bila ya kufahamu mafundisho yao mapya matakatifu. Akina Owen katika Uingereza, wanawapinga Chartists[18] na akina Fourier katika Ufaransa, wanawapinga Reformistes.[19]

IV

MSIMAMO WA WAKOMUNIST KUHUSU VYAMA MBALIMBALI VILIVYOKO VYA UPINZANI

 

Sehemu ya II imeelezea wazi msimamo wa wakomunist kuhusu vyama vya wafanya kazi vilivyoko, yaani kuhusu Chartists katika Uingereza na wafuasi wa mabadilisho katika kilimo huko Amerika.

Wakomunist wanapigania yapatikane madhumuni na masilaha ya sasa ya wafanya kazi; lakini, wakati huo huo, katika nyendo za sasa, wao pia huwakilisha na kuchukua hadhari уa wakati ujao wa nyendo hizo. Katika Ufaransa wakomunist wanaungana na Chama cha Demokrasi ya Kisoshialist,[20] kuwapinga mabepari wapendao kuhifadhi ya zamani na wapendao mabadilisho makubwa, lakini wakijiwekea haki yao ya kukosoa maneno na fikira za ndotoni ambazo asili yake zimerithiwa kutokana na desturi ya Thawra Kuu.

Katika Switzerland wanawaunga mkono wale wapendao mabadilisho makuu, bila ya kusahau kwamba chama hichi kimekusanya aina za watu wanaokabiliana, sehemu moja ni ya wasoshialist wa kidemokrasi wa namna ya Kifaransa, sehemu nyingine ni ya mabepari wapendao mabadilisho makuu.

Katika Poland wakomunist wanakiunga mkono chama kinachoshikilia ugeuzwaji mkuu katika kilimo kama ndio shuruti muhimu kwa ukombozi wa nchi, kile chama kilichochochea uasi wa Cracow katika mwaka 1846.

Katika Ujerumani chama cha kikomunist kinapigana pamoja na mabepari kila wanapofuata mwendo wa kithawra, kupinga utawala kamili wa mfalme, mali ya ardhi ya kibwanyenye na mabepari wadogo wa mijini wanaopinga maendeleo.

Lakini wakomunist hawajapatapo kusita hata mara moja kuwaelimisha wafanya kazi utambuzi wazi wazi kabisa unaoyumkinika wa uadui wa kihasimu ulioko baina ya mabepari na maproletarii, ili kwamba wafanya kazi waweze papo hapo kuzitumia hali za kijamaa na za kisiasa ambazo mabepari lazima wazianzishe pamoja na utawala wao, kama silaha ya kuwapinga mabepari wenyewe, na ili kwamba, baada ya uangukaji wa tabaka zipingazo maendeleo katika Ujerumani, vita dhidi ya mabepari wenyewe vianze papo hapo.

Macho ya wakomunist yameelekezea sana katika Ujerumani, kwani nchi hiyo imo ukingoni mwa thawra ya kibepari, kwani thawra hii itafanywa katika hali za mbele sana za ustaarabu wa Ulaya, ambapo wafanya kazi wamekua zaidi, kuliko wale waliokuwapo Uingereza katika karne ya kumi na saba, na Ufaransa katika karne ya kumi na nane. Kwa hivyo thawra ya kibepari katika Ujerumani itaweza kuwa ni kitangulizi tu kwa thawra ya wafanya kazi ifuatayo papo hapo.

Kwa ufupi, wakomunist kila mahali wanaunga mkono kila nyendo za kithawra zipingazo utaratibu wa kijamaa na wa kisiasa uliopo sasa.

Katika nyendo zote hizi wanaleta mbele swali la kumiliki mali kama ndilo swali muhimu zaidi katika kila nyendo, haidhuru vipi kiwe kipimo cha ukuaji wake wakati huo.

Mwishowe wakomunist wanajitahidi kila mahali kuleta umoja na mapatano ya vyama vya kidemokrasi vya nchi zote.

Wakomunist wanakirihika kuficha maoni na madhumuni yao. Wanatangaza wazi wazi kwamba madhumuni yao hayawezi kupatikana isipokuwa upinduliwe kwa nguvu utaratibu mzima wa ujamaa ulioko sasa. Ziacheni tabaka zinazotawala zitetemeke kwa kuogopa Thawra ya Kikomunist. Wafanya kazi hawana cho chote cha kuhofia kupoteza isipokuwa minyororo yao tu. Na wataiteka dunia nzima.

 

__________________

[1] Metternich, Clemens, Prince (1773-1859) - mwanasiasa wa Austria, mjumbe wa kiserikali, Waziri wa Mambo ya Nje (1809-1821) na Waziri Mkuu (1821-1848), mpingaji maendeleo mkubwa.

Guizot, Frangois Pierre Guillaume (1787-1874) - mtaalamu wa kibepari wa historia na mwanasiasa wa Ufaransa, kiongozi halisi wa siasa ya ndani na ya nje ya Ufaransa baina ya mwaka 1840 na 1848, mte tezi wa maslaha ya mabepari wakubwa wa fedha. (Mteng.)

[2] Neno hili mabepari maana yake ni tabaka ya makepitalist wa kisasa, wenye kumiliki zana za uchumi wa kijamaa na wenye kuajiri kazi ya kibarua. Maana ya maproletarii ni tabaka ya vibarua wa kisasa wafanyao kazi kwa ujira, ambao ilivyokuwa hawana zana zao wenyewe za uchumi, wamefikishwa hali ya kuuza uwezo wao wa kufanya kazi ill wapate kuishi. (Maelezo yaliyotolewa na Engels kwa Mchapo wa Kiingereza wa mwaka 1888.)

[3] Yaani, taarikh yote tangu ile iliyoandikwa. Katika mwaka 1847, ujamaa wa kabla ya taarikh, mpangiko wa ujamaa uliokuwako kabla ya taarikh iliyoandikwa ulikuwa wote haujulikani. Tangu wakati huo Haxthausen[21] amegundua aina ya kumiliki ardhi kwa pamoja (komyuni ya kijijini) katika Urusi, Maurer[22] aliihakikisha kwamba ilikuwa ni msingi wa kijamaa ambao ulikuwa ndio mwanzo wa maendeleo ya kitaarikh ya kabila zote za Teutonic na baadaye imeonekana kuwa komyuni ya kijijini, ambapo watu walikuwa wakimiliki ardhi pamoja, ni aina ya kikale ya ujamaa au ilikuwa zamani kila mahali kutoka Bara Hindi hadi Ireland. Mpangiko wa ndani wa ujamaa huu wa kikale wa kikomunist uliwekwa wazi, katika umbo lake hasa na uvumbuzi mwema wa Morgan[23] juu ya tabia ya kweli ya ukoo wa kuumeni na hali yake katika kabila. Kwa uvunjikaji wa jamii za kikale ujamaa unaanza kutofautishwa katika tabaka mbalimbali na mwishowe kuwa za kiadui. Nimejaribu kurejea nyuma mwendo huu wa mvunjiko katika kitabu kiitwacho: "Der Ursprung der Familie, des Privateigentums und des Staats" ("Asili ya Ukoo, Mali isiyokuwa ya wote na serikali".). Mchapo wa pili, Stuttgart, mwaka 1886. (Maelezo yaliyotolewa na Engels kwa mchapo wa Kiingereza wa mwaka 1888).

[4] Fundi wa ushirika wa wasanifu yaani mwanachama kamili wa ushirika, bwana aliyemo ndani yake wala si mkubwa wake. (Maelezo yaliyotolewa na Engels kwa kitabu cha Kiingereza cha mwaka 1888.)

[5] "Komyuni” ilikuwa ndilo jina lililochukuliwa katika Ufaransa na miji у a mwanzo hata kabla haikupata kutoka kwa mabwana zao serikali ya kienyeji ijiendeshayo wenyewe na haki za kisiasa za "tabaka ya tatu". Kwa kawaida, tukisema juu ya maendeleo ya iktisadi ya mabepari, Uingereza hapa inachukuliwa kama ndio mfano hasa wa nchi kama hiyo, na juu ya maendeleo yake ya kisiasa, Ufaransa ndiyo inachukuliwa kama ni mfano hasa.(Maelezo yaliyotolewa na Engels kwa mchapo wa Kiingereza wa mwaka 1888.)

Komyuni - hili ndilo jina lililopewa jamii zao za mjini na watu wa mjini wa Taliana na Ufaransa, baada ya kwisha kununua au kuzibakua haki zao za mwanzo za kujitawala wenyewe kutokana na mabwanyenye wao. (Maelezo yaliyotolewa na Engels kwa mchapo wa Kijerumani wa mwaka 1890.)

[6] Misafara ya Msalaba — misafara ya kivita у a kutaka makoloni iliyofanywa na mabwanyenye wa Magharibi chini ya kisingizio cha kuwaokoa watakatifu wa kikristo katika Uyahudi na "nchi takatifu" nyinginezo kutokana na utawala wa Waislamu. (Mteng.)

[7] Katika maandishi ya baadaye Marks na Engels walitumia badala ya maneno "thamani ya kazi", "bei ya kazi” maneno barabara zaidi yaliyoanzishwa na Marks: "thamani ya nguvu ya mfanya kazi", "bei ya nguvu ya mfanya kazi." (Mteng.)

[8] Siyo wakati wa kurejesha hali ya zamani katika Uingereza mwaka 1660 mpaka 1689, bali ni wakati wa kurejesha hali ya kizamani katika Ufaransa tangu mwaka 1814 mpaka 1830. (Maelezo hayo yametolewa na Engels kwa mchapo wa Kiingereza wa mwaka 1888.)

[9] Legitimist wa Kiiaransa - wafuasi wa ufalme wa Bourbon ambao uliuzuliwa katika mwaka 1830 na ambao uliwakilisha maslaha ya wenye miliki kubwa ya ardhi ya kurithi. Katika mapigano yao kuupinga ufalme unaotawala wa Orleans ambao ulitegemea juu ya kikundi cha wakubwa wenye fedha na mabepari wakubwa, sehemu ya legitimist walitumilia uwongo wakijidai kuupatia faida ujamaa na kujifanya kama walinzi wa watu wafanyao kazi kutokana na wanyonyaji damu wa kibepari. (Mteng.)

[10] Uingereza Changa - kikundi cha wanasiasa wa Kiingereza na waandishi waliokuwamo katika Chama cha Wahifadhi wa mambo ya zamani (the Tories). Kilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1840. Uingereza Changa kilionyesha kutotoshelezeka kwa watu wakubwa wenye ardhi juu ya nguvu ikuayo ya kisiasa na ya iktisadi ya mabepari. Wajumbe wake waliangukia kutumilia uwongo wakijidai kuupatia faida ujamaa na kujifanya kama ni walinzi wa tabaka ya wafanya kazi ili kuivuta iingie katika mapigano yao ya kuwapinga mabepari. (Mteng.)

[11] Haya yanakusudiwa sana Ujerumani ambako watu wakubwa wenye mashamba na mabwana shamba wanaendesha sehemu kubwa sana za mashamba yao kwa pesa zao wenyewe kwa njia ya watumishi, na, pia, ni wenye makarakana ya kutengeneza sukari ya kiazi na ulevi wa mbatata. Watu wakubwa wa Uingereza walio matajiri zaidi bado hawajalifikilia jambo hili; lakini wao, pia, wanajua, jinsi ya kujaliza mapato yaangukayo yanayotokana na kumiliki ardhi, kwa kutoa majina yao kama waanzishi wa makampuni yanayomilikiwa pamoja yenye kuendesha kazi za magendo. (Maelezo yametolewa na Engels kwa mchapo wa Kiingereza wa mwaka 1888.)

[12] Sismondi, Jean Charles Leonard Simonde (1773-1842) – bingwa wa iktisadi na mtaalamu wa historia wa Switzerland, aliukosoa ukepitalist kutokana na maoni ya mabepari wadogo. (Mteng.)

[13] Tufani ya kithawra ya mwaka 1848 iliufagia mtindo huo uliochakaa na kuwatibu waongozi wake hamu ya kutaka kuzidi kuutumilia usoshialist kwa faida yao. Mjumbe mkuu na mfano mwema wa mtindo huu ni Herr Karl Grun. (Maelezo yametolewa na Engels kwa mchapo wa Kijerumani wa mwaka 1890.)

[14] Proudhon, Pierre Josephe (1809-1865) - mwandishi wa Kifaransa, bingwa wa iktisadi na elimu ya ujamaa, mtaalamu wa mambo ya mawazo ya mabepari wadogo, mmoja miongoni mwa wazazi wa mawazo ya kutopendelea kuwapo utawala wo wote. Katika mwaka 1848, alichapa kitabu kiitwacho "Utaratibu wa Uadui wa Iktisadi, au Falsafa ya Ufukara" ambacho ndani yake alielezea maoni yake ya kibepari mdogo ya falsafa na iktisadi. Katika kitabu chake "Ufukara wa Falsafa" Marks kwa ukali sana alikikosoa kitabu cha Proudhon na kuhakikisha kwamba hakikuwa cha kisayansi kabisa. (Mteng.)

[15] Babeuf, Gracchus (jina lake la kweli Francois Noel) (1760-1797) - mwanathawra wa Kifaransa, mjumbe maarufu wa ukomunist wa usawa wa ndotoni. Alibuni jumuiya ya kisiri ambayo ilianza kutayarisha mapigano ya kutumia silaha yenye madhumuni ya kuanzisha utawala wa kithawra kwa ajili ya kuhifadhi maslaha ya umma mkubwa wa watu. Mipango hiyo ya kisiri iligunduliwa, na tarehe 27 Mei, 1797, Babeuf alinyongwa. (Mteng.)

[16] St. Simon, Henri-Claude (1760-1825) - mfuasi mkuu wa Kifaransa wa usoshialist wa ndotoni, aliukosoa utaratibu wa kikepitalist na kutoa mpango wa ubadilishwaji wake na ujamaa wenye msingi wa ushirika. Lakini St. Simon aliiacha vile vile bila ya kuigusa miliki isiyokuwa ya wote na faida ya rasilmali, alipinga mapigano ya kisiasa na thawra, akakosa kuufahamu ujumbe wa kitarehe wa tabaka ya wafanya kazi.

Fourier, Charles ((1772-1837) - mfuasi mkuu wa Kifaransa wa usoshialist wa ndotoni; alipinga thawra ya kutumia silaha na kuamini kwamba ukiukaji kuingia katika ujamaa ujao wa kisoshialist utafanyika kwa matokeo ya uenezi wa salama wa Phalansteres - shirikisho za kazi za kupigiwa mfano. Lakini Fourier hakuwa sawa kwa ilivyokuwa hakutaka iondoshwe miliki isiyokuwa ya wote, na tajiri na masikini, makepitalist na wafanya kazi walikuwa waishi pamoja katika shirikisho zake za kazi.

Owen, Robert (1771-1858) — mfuasi mkubwa wa Kiingereza wa usoshialist wa ndotoni.

Alikuwa na maoni kwamba sababu kubwa zaidi ya hali ya kutokuwa sawa katika ujamaa ilikuwa ni uenezaji usiotosha wa elimu na uongofu wala si aina ya kikepitalist ya utoaji wa bidhaa. (Mteng.)

[17] Phalansteres zilikuwa ni makoloni ya kisoshialist kwa mujibu wa mpango wa Charles Fourier: "Ikaria" ndilo jina lililotolewa na Cabet kuipa nchi yake ya ndotoni na baadaye koloni ya kikomunist ya Amerika. (Maelezo yametolewa 11a Engels kwa mchapo wa Kiingereza wa mwaka 1888).

Makoloni ya Nyumbani ndivyo Owen alivyokuwa akiziita aina za mifano za ujamaa wa kikomunist. Phalansteres lilikuwa ndilo jina lililopewa majumba yatumiwayo na watu wote kwa mujibu wa mpango wa Fourier. Ikaria lilikuwa ndilo jina lililopewa nchi iliyobuniwa ndotoni tu, ambayo makazi yake ya kikomunist yalisanifiwa na Cabet. (Maelezo yametolewa na Engels kwa mchapo wa Kijerumani wa mwaka 1890).

[18] Chartists, wafuasi wa Waraka wa Umma ("Charter") - nyendo za kithawra za umma za wafanya kazi wa Kiingereza, ambazo zilitokea kwa sababu ya hali zao ngumu na kukosa haki za kisiasa. Nyendo hizo zilianza mwishoni mwa miaka ya 1830 zilikuwa ni za aina ya mikutano ya hadharani na midhahara. Zilikuwa zikiendelea na kusita mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1850. Sababu kubwa kwa nini nyendo hizo zikashindwa ni huo ukweli kwamba zilikosa uongozi barabara wa kithawra na mpango wenye madhumuni wazi. (Mteng.)

[19] Reformistes (wafuasi wa mabadilisho madogo madogo) - waungaji mkono wa gazeti La Reiorme ambao walipigania uanzishwaji wa jamhuri na ufanywaji wa mabadilisho madogo madogo ya kidemokrasi na ya kijamaa. (Mteng.)

[20] Chama ambacho wakati huo kiliwakilishwa katika baraza la kutunga sheria na Ledru-Rollin, katika mambo ya uandishi - na Louis Blanc[24], katika magazeti ya kila siku - na gazeti la Reforme. Jina hilo la Demokrasi ya Kisoshialist lililovumbuliwa nao lilionyesha sehemu Fulani уa chama cha Kidemokrasi au cha Kijamhuri ambacho kimegusishwa kidogo na rangi ya usoshialist. (Maelezo yametolewa na Engels kwa mchapo wa Kiingereza wa mwaka 1888.)

[21] Haxthausen, August (1792-1866) - afisa na mwandishi wa Kiprussia, mtungaji wa kitabu juu ya rnabaki ya utaratibu wa komyuni katika mahusiano ya ardhi katika Urusi. (Mteng.)

[22] Maurer, Georg Ludwig (1790-1872) - mtaalamu mashuhuri wa kibepari wa historia wa Ujerumani, alichungua utaratibu wa kijamaa wa Ujerumani ya kikale na ya zama za kati. (Mteng.)

[23] Morgan Lewis Henry (1818-1881) - mtaalamu mashuhuri wa Kimarekani, na mchunguzi wa ujamaa wa kikale. (Mteng.)

Chama hicho katika Ufaransa ambacho kilijiita wakati huo Chama cha Demokrasi ya Kisoshialist kiliwakilishwa na Ledru-Rollin katika mambo ya siasa, na katika mambo ya uandishi kiliwakilishwa na Louis Blanc: kwa hivyo, basi kilitofautiana sana na demokrasi ya kisoshialist ya Kijerumani iliyopo sasa. (Maelezo yametolewa na Engels kwa mchapo wa Kijerumani wa mwaka 1890).

[24] Ledru-Rollin, Alexandre Auguste (1807-1874) - mwandishi wa Kifaransa na mwanasiasa. mmoja katika viongozi wa mabepari wadogo wafuatao demokrasi, mtengenezaji wa gazeti La Reforme, mwanachama wa Serikali ya Kujishikiza katika mwaka 1848.( Mteng.)

Blanc, Louis (1811-1882) - bepari mdogo wa Kifaransa afuataye usoshialist na mtaalamu wa historia; mwanachama wa Serikali ya Kujishikiza katika mwaka 1848 na mwenye kiti wa Komiti ya "Uchunguzi juu ya Swali la Wafanya Kazi", alitetea yafanywe mapatano na mabepari. (Mteng.)