Maelezo ya chama cha kikomunist

 

 

UTANGULIZI KWA MCHAPO WA KIJERUMANI WA MWAKA 1872

 

K. Marks & F. Engels

 


Tarehe ya kuandika: Katika juni 1872, kwa Karl Marx na Friedrich Engels.
Tarehe ya kuchapishwa: Katika 1872.
Toleo hili: Marxists Internet Archive (marxists.org),februari 2013.
Chanzo cha Nakala: Karl Marks na Frederick Engels, Maelezo y Chama cha Kikomunist, Moscow, Idara ya Maendeleo (1965).


 

 

"Umoja wa Wakomunist", jumuiya ya kilimwengu ya wafanya kazi, ambayo iliweza, bila ya shaka, kuwa ni ya siri tu katika hali zilizokuwapo wakati huo, imewapa kazi hao waliotia sahihi zao chini, kwenye mkutano mkuu uliofanywa London katika Novemba mwaka 1847, kutengeneza kwa ajili ya kuchapwa mpango wazi wa mawazo na matendo ya Chama. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa "Maelezo" yafuatayo, ambayo maandishi yake yalisafirishwa mpaka London yapigwe chapa, wiki chache kabla ya Thawra ya Februari.[1] Mwanzo yalipigwa chapa kwa Kijerumani na yakapigwa chapa tena kwa lugha hiyo hiyo si chini kuliko mara kumi na mbili katika Ujerumani, Uingereza na Amerika. Yalifasiriwa kwa Kiingereza na bibi Helen Macfarlane na yalichapwa kwa mara ya mwanzo mwaka 1850 katika gazeti liitwalo Red Republican, huko London, na katika mwaka 1871 kwa tafsiri mbalimbali zisizopungua chini ya tatu katika Amerika. Tafsiri ya Kifaransa ilichapwa mwanzo katika Paris punde kabla ya uasi wa Juni ya mwaka 1848 na karibuni katika gazeti la New York liitwalo Le Socialiste. Tafsiri mpya imo katika kutayarishwa. Tafsiri kwa lugha ya Kipolish ilichapwa London punde baada ya kuchapwa kwa mara ya mwanzo kwa Kijerumani. Tafsiri kwa lugha ya Kirusi ilipigwa chapa Geneva katika miaka ya 1860. Pia yalifasiriwa kwa lugha ya Kidenish, baada ya kutokeza kwa mara ya kwanza.

Ingawaje hali ya mambo inavyokuwa imebadilika sana katika muda wa miaka ishirini na tano iliyopita, lakini fikira za msingi zilizowekwa katika "Maelezo" haya, kwa vikubwa, ni sahihi leo kama zilivyokuwa zamani. Hapa na pale baadhi ya mambo madogo madogo yanaweza kutengenezwa. Utekelezwaji kwa matendo wa fikira hizo za msingi utategemea, kama "Maelezo” yenyewe yanavyosema, kila mahali na wakati wote, juu ya hali za kitaarikh zinazokuwapo wakati huo, na, kwa sababu hiyo, hatua za kithawra zilizoshauriwa kuchukuliwa mwishoni mwa Sehemu ya II si hatua zenye kulazimu kwa nchi zote. Kwa hali nyingi, sehemu ile ingaliandikwa vingine leo. Kwa sababu ya usitawi mkubwa uliopatikana katika uchumi wa kisasa kwa muda wa miaka 25 iliyopita na kufuatia hayo jumuiya iliyotanuka na kutengenea zaidi ya tabaka ya wafanya kazi; kwa sababu ya maarifa hasa waliyoyapata, mwanzo katika Thawra ya Februari, na baadaye mengi zaidi, katika Komyuni ya Paris, ambapo wafanya kazi kwa mara ya mwanzo waliikamata serikali kwa miezi miwili mizima, mpango huo katika baadhi ya mambo madogo madogo umekuwa ni wa kizamani. Hasa Komyuni imethibitisha kwamba "tabaka ya wafanya kazi haiwezi tu kuyakamata madaraka ya kiserikali yaliyokwisha tayarishwa zamani na kuyatumia kwa madhumuni yao wenyewe." (Tazama "Der Biirgerkrieg in Frankreich, Adresse des Generalrats der Intemationalen Arbeiterassoziation", Mchapo wa Kijerumani, uk. 19, ambapo mambo haya yanaelezewa zaidi[2].) Zaidi, inaonekana wenyewe, kwamba utoaji wa makosa kwa maandishi ya kisoshialist haukukamilia kuhusu wakati wa sasa, kwa sababu unakuja mpaka mwaka 1847 tu; pia, maelezo juu ya msimamo wa wakomunist kwa vyama mbalimbali vya upinzani (Sehemu IV), ingawa kwa msingi bado yangali barabara, lakini kwa sehemu zake nyingine yameshakuwa hayafai tena, kwani hali ya kisiasa imebadilishwa kabisa, na maendeleo ya taarikh yamefagia duniani sehemu kubwa ya vyama vilivyotiwa hesabuni hapo.

Lakini basi, "Maelezo" haya yamekuwa ni waraka wa kitaarikh ambao hatuna tena haki yo yote ya kuubadilisha. Pengine kwa mchapo ujao tutafaulu kuandika utangulizi wenye kuelezea wakati huo kutoka mwaka 1847 mpaka wakati huu wa sasa; kuchapwa kwa kitabu hiki kulitokea kwa ghafla sana hata hatukupata wakati wa kufanya hayo.

Karl Marks. Frederick Engels

London, tarehe 24 Juni, 1872

_________________

[1] Thawra ya Februari katika Ufaransa mwaka 1848. (Mleng.)

[2] Tazama K. Marks. “ Vita vya Nchini katika Ufaransa. Uwito wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wafanya Kazi wa Dunia." (Mteng.)