Maelezo ya chama cha kikomunist

 

 

UTANGULIZI KWA MCHAPO WA KIJERUMANI WA MWAKA 1883

 

F. Engels

 


Tarehe ya kuandika: Katika juni 1883, kwa Friedrich Engels.
Tarehe ya kuchapishwa: Katika 1883.
Toleo hili: Marxists Internet Archive (marxists.org),februari 2013.
Chanzo cha Nakala: Karl Marks na Frederick Engels, Maelezo y Chama cha Kikomunist, Moscow, Idara ya Maendeleo (1965).


 

 

Ninasikitika kusema kuwa utangulizi wa mchapo huo wa sasa lazima niutie sahihi реке yangu. Marks, mtu ambaye tabaka nzima ya wafanya kazi katika Ulaya na Marekani inamwia yeye kuliko mtu ye yote mwingine - hivi sasa amelala katika kiunga cha Highgate na juu ya kaburi lake majani yameshaanza kuota. Tangu kufa kwake, ndio zaidi hapatakuwa na fikira ya kuyabadilisha au kuyaongeza "Maelezo" hayo. Ndio zaidi ninahisi kuwa inahitajia tena kuyaelezea hapa haya yafuatayo kwa maana yake halisi.

Fikira kuu iliyomo ndani ya "Maelezo" hayo - kwamba utoaji wa iktisadi na umbo la ujamaa wa kila zama za kitaarikh ambalo lazima linatokana nao, yote mawili ndiyo yenye kufanya msingi wa historia ya kisiasa na ya akili ya zama hizo; kwamba kwa mujibu wa hayo (tangu wakati ulipovunjwa utaratibu wa kikale wa kumiliki ardhi kwa pamoja) taarikh yote imekuwa ni taarikh ya mapigano ya kitabaka, ya mapigano kati ya wanyonywao damu na wale wanaonyonya, kati ya tabaka zitawaliwazo na zile zenye kutawala katika daraja mbalimbali za maendeleo ya ujamaa; kwamba mapigano hayo, ingawaje, hivi sasa yameshafika katika daraja ambapo tabaka ya wanyonywao damu na wakandamizwao (tabaka ya wafanya kazi) haiwezi tena kujiokoa nafsi yake kutokana na tabaka iwanyonyayo damu na kuwakandamiza (tabaka ya mabepari), bila ya pia kuuokoa milele ujamaa mzima kutokana na unyonyaji damu na ukandamizo na mapigano ya kitabaka - fikira hii kuu si ya mwinginewe ye yote isipokuwa ni ya Marks pekee.[1]

Nimeshaelezea haya mara nyingi, lakini hasa sasa inahitajia kwamba tangazo hili liwekwe mbele ya "Maelezo" yenyewe.

F. Engels

London, tarehe 28 Juni, 1883

____________________________________

[1] "Fikira hii," niliandika katika utangulizi kwa tafsiri ya Kiingereza, ambayo, kwa maoni yangu, imekusudiwa kuwa na maana ile ile kwa taarikh kama yalivyo mawazo ya Darwin[2] kwa elimu ya viumbe, sisi, sote wawili, tumekuwa tukiikurubia pole pole kwa miaka kadha tangu kabla ya mwaka 1845. Umbali gani mimi реке yangu nimeendelea kuifikia, unaonekana vizuri Sana katika maandishi yangu: Hali ya tabaka ya wafanya kazi katika Uingereza. Lakini nilipokutana naye tena Marks katika mji wa Brussels, katika majira ya Spring, mwaka 1845, alikuwa ameshaibuni, na kuniletea mbele yangu, kwa maelezo wazi kabisa yanayokurubia sana na hayo niliyoyaelezea hapa." (Maelezo ya.liyoand.ikwa na Engels kwa mchapo wa Kijerumani wa mwaka 1890).

[2] Darwin, Charles Robert (1809-1882) - mtaalamu mkuu wa Kiingereza, mzumbuzi wa elimu ya viumbe kwa kufuata mawazo ya materialism (mambo yaliyopo) na mawazo ya mabadiliko ya pole pole ya asili ya viumbe na mimea kwa njia ya uchunguzi wa maumbile.

"Darwin alikomesha mawazo ya kuona aina za viumbe na mimea kama ni za bahati tu na ambazo hazikushikamana, zilizoumbwa na Mungu na zisizobadilika, na alikuwa wa mwanzo kuiweka elimu ya viumbe juu ya msingi wa kisayansi kabisa kwa kuanzisha fikira ya mbadiliko na mfuatano wa aina za viumbe. . (V. I. Lenin) - (Mteng.)