Maelezo ya chama cha kikomunist

 

 

UTANGULIZI KWA MCHAPO WA KIINGEREZA WA MWAKA 1888

 

F. Engels

 


Tarehe ya kuandika: Katika juni 1888, kwa Friedrich Engels.
Tarehe ya kuchapishwa: Katika 1888.
Toleo hili: Marxists Internet Archive (marxists.org),februari 2013.
Chanzo cha Nakala: Karl Marks na Frederick Engels, Maelezo y Chama cha Kikomunist, Moscow, Idara ya Maendeleo (1965).


 

 

"Maelezo” yalitangazwa kama ndiyo mpango wa "Umoja wa Wakomunist” , jumuiya ya wafanya kazi, ambayo mwanzoni ilikuwa ya Wajerumani tu, na baadaye ya dunia nzima, na katika hali za kisiasa zilizokuwapo Ulaya kabla ya mwaka 1848, ilibidi iwe jumuiya ya siri. Kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja huo uliofanywa London katika mwezi wa Novemba, mwaka 1847, Marks na Engels walipewa kazi ya kutayarisha ili utangazwe mpango kamili wa mawazo na wa matendo ya Chama. Ulitungwa katika Januari, mwaka 1848, na maandishi yake уa Kijerumani yakapelekwa kuchapwa London, wiki chache kabla ya Thawra ya Ufaransa у a tarehe 24 Februari. Tafsiri ya Kifaransa ilitolewa katika Paris punde kabla ya kufanywa thawra ya Juni, mwaka 1848. Tafsiri ya mwanzo ya Kiingereza iliyofanywa na Bibi Helen Macfarlane, ilitokeza katika gazeti la George Julian Harneys liitwalo Red Republican, katika mji wa London mwaka 1850. Pia yalichapwa kwa lugha ya Kidenish na Kipolish.

Kushindwa kwa thawra ya Paris ya Juni, mwaka 1848 - vita vikali vya mwanzo kati ya tabaka ya wafanya kazi na ya mabepari - kuliyapeleka tena nyuma, kwa muda fulani, matakwa ya kijamaa na у a kisiasa у a tabaka у a wafanya kazi wa Ulaya. Tangu wakati huo, mapiganio ya kutaka utawala yakawa tena, kama yalivyokuwa kabla ya thawra ya Februari, baina у a sehemu mbalimbali za wenye mali tu; wafanya kazi walilazimishwa kupigania uhuru wa kisiasa wa matendo na kuchukua msimamo wa upande mkali wa tabaka ya wenye hali ya wastani wanaotaka mabadilisho makuu. Po pote pale zilipoonekana nyendo za wafanya kazi реке yao zinaendelea kuonyesha dalili za uhai, zilisakwa na kufyekwa kwa ukatili. Basi hivyo ndivyo maaskari wa Prussia walivyoisaka Komiti Kuu уa Umoja wa Wakomunist, ambayo wakati huo ilikuwapo katika Cologne. Wanachama walikamatwa na baada ya kutiwa ndani kwa miezi kumi na nane ndipo wakahukumiwa katika Oktoba, mwaka 1852. "Kesi ya Wakomunist katika Cologne" inayojulikana sana ilianza tangu tarehe 4 Oktoba ikamalizikia tarehe 12 Novemba; wafungwa saba katika hao walihukumiwa kufungwa katika ngome kwa muda unaoanzia tangu miaka mitatu hadi sita. Papo hapo baada ya kukatwa hukumu hiyo, Umoja wa Wakomunist ulifungwa rasmi na wanachama waliobakia. Ama kwa "Maelezo" ilionekana kama kwamba yameangamia kupotea kabisa.

Wakati tabaka ya wafanya kazi wa Ulaya ilipokwisha pata nguvu tena za kutosha kufanya shambulio jingine kwa tabaka zinazotawala, Jumuiya ya Wafanya kazi wa Dunia yaani Interantional ilichipuka. Lakini Jumuiya hii iliyoundwa kwa madhumuni hasa ya kuziunganisha nguvu zote za wafanya kazi zilizoweza kupigana za Ulaya na Amerika kuwa kitu kimoja, haikuweza papo hapo kuzitangaza kanuni zilizowekwa katika "Maelezo". Jumuiya hiyo ya Dunia ilibidi iwe na mpango uliotandaa sana hata kuweza kukubaliwa na vyama vya wafanya kazi vya Uingereza, na wafuasi wa Proudhon[1] katika Ufaransa, Ubelgiji, Taliana, na Spain, na wafuasi wa Lassale[2] katika Ujerumani. Marks, ambaye ndiye aliyeutunga mpango huo kwa kuvitosheleza vyama vyote hivi, aliaminisha kabisa juu ya ukuaji wa akili ya wafanya kazi, ambao ulikuwa lazima utokee baada ya matendo ya pamoja na mashauriano. Matukio na mageuzi yenyewe ya mapigano dhidi ya rasilmali - kushindwa hata zaidi kuliko kushinda - yalisababisha kuwafahamisha wafanya kazi juu ya upungufu wa njia zao mbalimbali wazipendazo za kuleta nafuu, na kufagia njia kwa ajili ya ufahamu kamili zaidi katika mashuruti ya kweli у a ukombozi wa tabaka ya wafanya kazi. Na Marks hakukosea. Jumuiya hiyo ya Dunia, ilipovunjika katika mwaka 1874, iliwaacha wafanya kazi wa namna nyingine kabisa wasiofanana na wale iliyowakuta katika mwaka 1864. Mawazo ya Proudhon katika Ufaransa na Lassale katika Ujerumani yalikuwa yakififia, na hata vyama vya wafanya kazi vyenye kuhifadhi desturi za zamani vya Uingereza, ingawa vingi katika hivyo vilikuwa vimeshavunja muungano wao na Jumuiya hiyo ya Dunia, vilikuwa pole pole vikienda mbele kufika hadi ambapo mwaka jana katika mkutano huko Swansea, Rais wao aliweza kusema kwa niaba yao: "Usoshialist wa Kontinenti haututishi tena sisi” . Kwa hakika: kanuni za “Maelezo” zimefanya maendeleo makubwa miongoni mwa wafanya kazi wa nchi zote.

"Maelezo” yenyewe kwa hivyo yakaja mbele tena. Kitabu cha Kijerumani kimekuwa tangu mwaka 1850 kikichapwa tena na tena mara kadha katika Switzerland, Uingereza na Amerika. Katika mwaka 1872, kilifasiriwa kwa Kiingereza katika mji wa New York, ambako tafsiri hiyo ilichapwa katika jarida la Woodhull and Clatliris Weekly. Kutokana na tafsiri hii ya Kiingereza, tafsiri ya Kifaransa ikafanywa na ikachapwa katika gazeti Le Socialiste la New York. Tangu wakati huo hazipungui chini ya tafsiri mbili za Kiingereza, zilizoharibiwa kidogo, zilitolewa katika Amerika, na mo ja katika hizo ilipigwa chapa tena katika Uingereza. Tafsiri ya kwanza ya Kirusi, iliyofanywa na Bakunin, ilichapwa kwenye nyumba ya kuchapia vitabu ya Hertzen Kolokol katika Geneva, kiasi mwaka 1863; ya pili, iliyofanywa na shujaa Vera Zasulich[3] ilichapwa pia katika Geneva, mwaka 1882. Kitabu kipya kwa lugha ya Kidenish kinaweza kuonekana katika Social-democratisk Bibliothek, Copenhagen, mwaka 1885; tafsiri mpya ya Kifaransa ilichapwa katika gazeti Le Socialiste, Paris, mwaka 1886[4]. Kutokana na hiyo ya mwisho ilifanywa tafsiri у a Kispanish na kuchapwa katika mji wa Madrid, mwaka 1886. Tusivitie hesabuni vitabu vilivyochapwa tena na tena kwa Kijerumani, kwa uchache mara zote pamoja ni kumi na mbili. Tafsiri ya Kiarmenia iliyobidi kuchapwa miezi kadha iliyopita, katika Constantinople, haikupata kutokeza, nimeambiwa, kwa sababu mchapaji aliogopa kutoa kitabu cho chote chenye jina la Marks, ambapo mtu aliyefasiri alikataa kukiita kuwa kitabu ohake mwenyewe. Nimesikia juu ya tafsiri nyingi zaidi kwa lugha nyingine, lakini mimi mwenyewe sikuziona. Kwa hivyo basi taarikh ya "Maelezo” inaonyesha, kwa vikubwa sana kuwa ni taarikh ya nyendo za kisasa za tabaka уa wafanya kazi; kwa sasa, bila ya shaka, yameenea sana na yanachapwa katika sehemu nyingi sana za dunia kupita maandishi yo yote ya kisoshialist, na yamekuwa ni mpango wa pamoja unaokubaliwa na mamilioni ya wafanya kazi kutoka Siberia hadi California.

Juu ya hivyo, wakati yalipoandikwa, hatukuweza kuyaita Maelezo ya Kisoshialist. Kwani kwa kutumia neno hili Masoshialist, katika mwaka 1847, ilifahamika, kwa upande mmoja, kuwa ni wafuasi wa taratibu za aina mbalimbali za ndotoni: akina Owen katika Uingereza, akina Fourier katika Ufaransa, na wakati ule, zote hizo zimeshafikishwa hali ya kuwa mafarakano tu, na pole pole zinaanza kufifia; kwa upande mwingine, zilikuwa ni aina nyingi sana za waganga wanaojidai kutaka kuuletea nafuu ujamaa, ambao kwa njia ovyo za kuziba ziba walijinata kuyaondosha maafa yote ya ujamaa bila ya kuihatarisha hata kidogo rasilmali na faida. Katika hali zote mbili wao walikuwa ni watu walioko nje ya nyendo za wafanya kazi, na wenye kuzitegemea sana tabaka za "waliosoma" kwa kupata msaada. Pande jingine la tabaka ya wafanya kazi lililokuja kuamini juu ya upungufu wa thawra tupu za kisiasa tu na likatangaza haja ya kubadilishwa kabisa ujamaa mzima, lilijiita wakomunist. Ulikuwa ni aina ya ukomunist usio safi, uliobubutika na wenye kusababishwa na hisi ya ndani ya nafsi tu; hata hivyo, uligusa jambo muhimu na umekuwa na nguvu za kutosha miongoni mwa wafanya kazi kuweza kuleta ukomunist wa ndotoni, wa Cabet[5] katika Ufaransa na wa Weitling[6] katika Ujerumani. Basi, usoshialist ulikuwa, katika mwaka 1847, ni mwendo wa tabaka ya mabepari, na ukomunist ukawa ndio mwendo wa tabaka ya wafanya kazi. Usoshialist katika Kontinenti ulikuwa "unaheshimiwa"; ukomunist ulikuwa ni kinyume chake kabisa. Na kama fikira yetu i-livyokuwa, tangu mwanzo, kwamba "ukombozi wa tabaka ya wafanya kazi lazima uwe ni tendo la wafanya kazi wenyewe tu,” hapangaliweza kuwa na shaka у о yote ya jina gani katika hayo mawili inatupasa tuchukue. Zaidi ya hayo, baadaye pia hatukuwa tukilikataa.

"Maelezo” haya yakiwa ni kazi yetu ya pamoja, ninajihisi imenipasa nielezee kwamba fikira muhimu, ambayo ndiyo kiini cha "Maelezo” hayo, inatokana na Marks. Fikira yenyewe ni: kwamba katika kila zama za kitaarikh, aina kubwa inayokuwapo ya utoaji wa iktisadi na mabadilishano ya bidhaa, na mpangiko wa ujamaa ambao lazima unafuata kutokana nayo, vyote pamoja vinaanzisha msingi ambao juu yake inajengwa na kutokana nao tu pekee ndipo inapoweza kuelezewa, taarikh ya kisiasa na maendeleo ya akili ya zama hizo; kwamba kwa mujibu wa hayo, taarikh yote уa mwanadamu (tangu baada уa kuvunjika kwa ujamaa wa kikale wa kikabila, wenye kuimiliki ardhi kwa pamoja) imekuwa ni taarikh ya mapigano baina ya tabaka, mapigano baina ya wanyonyaji na wanyonywao damu, wanaotawala na wanaokandamizwa; kuwa taarikh ya mapigano haya ya kitabaka siku hizi imefika daraja ambapo tabaka inyonywayo damu na kukandamizwa - tabaka ya wafanya kazi - haiwezi kupata ukombozi wake kutokana na nguvu za tabaka inyonyayo damu na kutawala - tabaka уa mabepari - bila ya kuukomboa ujamaa wote kutokana na aina zote za unyonyaji damu, mkandamizo, tofauti za kitabaka na mapigano ya kitabaka, kwa mara moja na ya mwisho.

Fikira hiyo, ambayo kwa maoni yangu, ina maana ile ile kwa taarikh kama yalivyo mawazo у a Darwin kwa elimu у a viumbe, sisi sote wawili, tumekuwa taratibu tukiikurubia kwa miaka kadha kabla ya mwaka 1845. Umbali gani nimeendelea реке yangu kuifikilia unaonyeshwa vizuri katika maandishi yangu juu ya Hali za tabaka у a wafanya kazi katika Uingereza.[7] Lakini nilipokutana tena na Marks katika Brussels, wakati wa majira ya Spring, mwaka 1845, alikuwa ameshaitunga, na kuniwekea mbele yangu kwa maelezo wazi sana kama yale niliyoyaelezea hapa.

Kutoka katika utangulizi tuliouandika pamoja kwa mchapo wa Kijerumani wa mwaka 1872 nitanukulu haya yafuatayo:

"Ingawaje hali ya mambo inavyokuwa imebadilika sana katika muda wa miaka ishirini na tano iliyopita, lakini fikira za msingi zilizowekwa katika "Maelezo" haya, kwa vikubwa, ni sahihi leo kama zilivyokuwa zamani. Hapa na pale baadhi ya mambo madogo madogo yangeweza kutengenezwa. Utekelezwaji kwa matendo wa fikira hizo za msingi utategemea, kama "Maelezo" yenyewe yanavyosema, kila mahali na wakati wote, juu ya hali za kitaarikh zinazokuwapo wakati huo, na, kwa sababu hiyo, hatua za kithawra zilizoshauriwa kuchukuliwa mwishoni mwa Sehemu ya II, si hatua zenye kulazimu kwa nchi zote. Kwa hali nyingi, sehemu ile ingaliandikwa vingine leo. Kwa sababu ya usitawi mkubwa uliopatikana katika uchumi wa kisasa tangu mwaka 1848 na kufuatia hayo jumuiya iliyotanuka na kutengenea zaidi ya tabaka ya wafanya kazi; kwa sababu ya maarifa hasa waliyoyapata, mwanzo katika Thawra ya Februari, na baadaye mengi zaidi, katika Komyuni ya Paris, ambapo wafanya kazi kwa mara ya mwanzo waliikamata serikali kwa miezi miwili mizima, mpango huo katika baadhi ya mambo madogo madogo umekuwa ni wa kizamani. Hasa Komyuni imethibitisha kwamba "tabaka ya wafanya kazi haiwezi tu kuyakamata madaraka ya kiserikali yaliyokwisha tayarishwa zamani na kuyatumia kwa madhumuni yao wenyewe." (Tazama "The Civil War in France; Address of the General Council of the International Working-men's Association". London, Truelove, 1871, uk. 15,[8] ambapo mambo haya yanaelezewa zaidi.) Zaidi inaonekana wenyewe, kwamba utoaji wa makosa kwa maandishi ya kisoshialist haukukamilia kuhusu wakati wa sasa, kwa sababu unakuja mpaka mwaka 1847 tu; pia, maelezo juu ya msimamo wa wakomunist kwa vyama mbalimbali vya upinzani (Sehemu IV), ingawa kwa msingi bado yangali barabara, lakini kwa sehemu zake nyingine yameshakuwa hayafai tena, kwani hali ya kisiasa imebadilishwa kabisa, na maendeleo ya taarikh yamefagia duniani sehemu kubwa ya vyama vilivyotiwa hesabuni hapo.

Lakini basi, "Maelezo” haya yamekuwa ni waraka wa kitaarikh ambao hatuna tena haki yo yote ya kuubadilisha.

Tafsiri hii ya sasa imefanywa na Bw. Samuel Moore, mtu aliyefasiri sehemu kubwa sana ya kitabu cha Marks kiitwacho Rasilmali. Tumeipitia pamoja, na nimeongeza maelezo machache yenye kuelezea matokeo ya kitaarikh.

Frederick Engels

London, tarehe 30 Jannuari, 1888.

___________________

[1] Tazama maelezo ya uk. 66 [katika toleo la 1965 katika Swaihili kutoka Idara  ya Maendeleo - Moscow (MIA)] (Mteng.) 

[2] Lassale binafsi yake, kwetu sisi, siku zote alijiita kuwa ni mfuasi wa Marks, na kwa hivyo, anasimama kuyafuata "Maelezo". Lakini katika mabishano yake mbele ya watu, 1862-1864, hakupindukia zaidi ya kudai uanzishwaji wa viwanda vya ushirika vyenye kusaidiwa kwa mikopo ya Serikali. (Maelszo yametanywa na Engels)

[3] Tafsiri hiyo haikufanywa na Vera Zasulich bali na G. V. Plekhanov, kama ilivyokuja onyeshwa barabara baadaye na Engels mwenyewe katika maelezo ya nyongeza kwa makala iitwayo "Mahusiano ya Kijamaa katika Urusi". Katika mchapo wa mwaka 1900 wa "Maelezo" hayo G. V. Plekhanov pia alionyesha kwamba yeye mwenyewe ndiye aliyefasiri.

Plekhanov, Georgii Valentinovich (1856-1918) - mtu mashuhuri katika nyendo za wafanya kazi za Urusi na za dunia, mwenezi wa mwanzo wa mafunzo ya Marks katika Urusi. Baada ya mwaka 1903 akawa mfuasi wa Umenshevik (mtindo wa ugeugeu katika Chama cha Demokrasi ya Kisoshialist cha Urusi). (Mteng.)

[4] Mwaka haukudhihirishwa wazi. "Maelezo ya Chama cha Kikomunist" yalifasiriwa kwa Kifaransa na Bibi Laura Lafarge na kuchapwa katika gazeti "Le Socialiste" tarehe 29 Agosti — 7 Novemba, 1885. (Mteng.)

[5] Cabet, Etienne (1788-1856) - mwandishi wa mabepari wadogo wa Kifaransa, mwakilishaji mashuhuri wa ukomunist wa ndotoni. Aliamini kwamba maovu ya utaratibu wa kibepari yanaweza kuondoshwa kwa ubadilishwaji wa salama wa ujamaa. Aliyaelezea maoni yake katika kitabu kiitwacho "Safari kwendea Ikaria (1840) na akayaribu kuyatekeleza kwa matendo kwa kuanzisha Komyuni ya Kikomunist katika Amerika, walakini majaribio yake hayakufaulu kamwe. (Mteng.)

[6] Weitling, Wilhelm (1808-1871) - mtu mashuhuri katika nyendo za tabaka у a wafanya kazi wa Ujerumani к wenye daraja zake za mwanzo, mmoja katika watungaji wa mawazo ya ukomunist wa ndotoni wa usawa, kazi yake alikuwa ni mshoni. (Mteng.)

[7] "The Condition of the Working Class in England in 1844". Kimeandikwa na Frederick Engels, kimefasiriwa na Florence K. Wischnewetzky, New York. Lovell - London. W. Reeves, mwaka 1888. (Maelezo yametolewa na Engels.)

[8]Tazama Karl Marks, Vita vya Nchini katika Ufaransa. Mwito wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wafanya Kazi wa Dunia. (Mteng.)