Maelezo ya chama cha kikomunist

 

 

UTANGULIZI KWA MCHAPO WA KITLIANA WA MWAKA 1893

 

F . E n g e l s

 

 


Tarehe ya kuandika: Katika juni 1893, kwa  Friedrich Engels.
Tarehe ya kuchapishwa: Katika 1893.
Toleo hili: Marxists Internet Archive (marxists.org),februari 2013.
Chanzo cha Nakala: Karl Marks na Frederick Engels, Maelezo y Chama cha Kikomunist, Moscow, Idara ya Maendeleo (1965).


 

 

KWA MSOMAJI WA KITALIANA

Uchapaji wa Maelezo ya Chama cha Kikomunist umetokea kwa bahati, mtu anaweza kusema, karibu na tarehe 18 Machi mwaka 1848, siku уa Thawra katika Milan na Berlin, ambazo zilikuwa ni mapigano ya silaha ya nchi mbili hizo zilizokuwa katikati, moja katika Kontinenti la Ulaya na ya pili katika nchi za Mediterranean; nchi mbili ambazo mpaka wakati huo zilidhoofishwa kwa migawiko na matata ya ndani, na kwa hivyo zikaangukia chini уa utawala wa kigeni. Wakati Taliana ilipokuwa ikitawaliwa na mfalme wa Austria, Ujerumani ilikuwa katika utumwa wa mfalme wa Urusi yote, wenye nguvu kama hizo ingawa ulikuwa kwa kificho zaidi. Natija ya matokeo ya tarehe 18 Machi, mwaka 1848, yaliziokoa zote Taliana na Ujerumani kutokana na aibu hii; ikiwa tangu mwaka 1848 mpaka 1871 mataifa hayo makubwa yamefufuliwa tena na vyo vyote vile yameanza tena kujiendesha wenyewe, ilikuwa, kama Karl Marks alivyokuwa akisema, kwa sababu watu walioididimiza Thawra ya mwaka 1848 walikuwa, juu ya hivyo, ndio waliotekeleza nia zake bila ya hiari zao wenyewe.

Kila mahali thawra imekuwa ni kazi ya wafanya kazi; wao ndio waliojenga maboma na kujihasirisha maisha yao. Lakini wafanya kazi wa Paris tu, katika kuipindua serikali, walikuwa na kusudio maalum la kuuondosha utaratibu wa mabe- pari. Lakini ijapokuwa walifahamu uadui usioepukika uliokuwapo kati yao na mabepari, ama si maendeleo ya iktisadi wala daraja ya fahamu ya umma wa wafanya kazi wa Kifaransa bado haikufika daraja ambayo ingaliuwezesha ujengwaji tena wa ujamaa. Katika uchambuzi wa mwisho, kwa hivyo, matunda ya thawra yalichumwa na tabaka ya makepitalist. Katika nchi nyinginezo, katika Taliana, katika Ujerumani, katika Austria, wafanya kazi, tangu mwanzo, hawakufanya cho chote isipokuwa kuwakweza mabepari serikalini. Lakini ко kote kule utawala wa mabepari hauyumkiniki bila ya kupatikana uhuru wa nchini. Kwa hivyo Thawra ya mwaka 1848 imebidi ilete, kama ni natija yake, umoja na kujitawala wenyewe kwa nchi ambazo hazikuwa nako mpaka wakati huo: Taliana, Ujerumani na Hungary. Poland nayo pia itafuata.

Basi, ikiwa Thawra ya mwaka 1848 haikuwa ya kisoshialist iliifagilia njia na kutayarisha mambo kwa hiyo ya pili. Utaratibu wa mabepari uliosababisha ukuaji wa uchumi mkubwa sana katika nchi zote, pamoja na hayo katika muda wa miaka arobaini na tano iliyopita umesababisha kila mahali kuwapo wafanya kazi wengi waliokusanyika pamoja na wenye nguvu sana. Kwa hivyo, tukitumia maneno ya "Maelezo” , utaratibu wa mabepari ulizaa wachimbaji makaburi yao wenyewe. Bila ya kupatikana kujitawala wenyewe na umoja kwa kila nchi, haitawezekana kupata muungano wa wafanya kazi wa dunia, wala mashirikiano ya salama na yenye fahamu ya nchi hizi kuendea malengo ya pamoja. Hebu kisia tendo la pamoja la kidunia lifanywalo na wafanya kazi wa Kitaliana, Kihungary, Kijerumani, Kipoland, na wa Kirusi katika hali za kisiasa zilizokuwepo kabla ya mwaka 1848!

Vita vilivyopiganwa katika mwaka 1848, kwa hivyo havikupotea bure. Wala muda wa miaka arobaini na tano uliotutenga sisi na zama zile za kithawra haukupita bila ya madhumuni yo yote. Matunda yake yanaiva, na yote ninayotamani ni kwamba uchapaji wa tafsiri hii ya Kitaliana utabashiri vile vile ushindi wa wafanya kazi wa Kitaliana kama ulivyofanya uchapaji wa maandishi ya asili kwa thawra ya dunia nzima.

"Maelezo” yanaelezea kwa ukamilifu kazi ya kithawra iliyofanywa na ukepitalist katika siku za nyuma. Nchi ya mwanzo ya kikepitalist ilikuwa ni Taliana. Mwisho wa ubwanyenye wa zama za kati na mwanzo wa zama za kisasa za kikepitalist umewekewa alama ya mtu mkubwa kabisa: Mtaliana Dante, mshairi wa mwisho wa zama za kati na pia ni mshairi wa mwanzo wa zama mpya. Leo, kama ilivyokuwa katika mwaka 1300, zama mpya za kitaarikh zinasonga mbele. Je, Taliana itatuletea Dante mpya atakayeiadhimisha saa ya kuzaliwa kwa zama hizi mpya, zama za wafanya kazi?

Frederick Engels

London, tarehe 1 Februari, 1893